WALIMU ACHENI ADHABU YA FIMBO

Tabia hii ya walimu irekebishwe mapema



Kwa ufupi

Mwalimu huyo alichukua hatua hiyo baada ya mwanafunzi kuharibu kifaa cha kuhifadhia gundi aliyoomba kwa ajili ya kuunganisha godoro lake.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeifunga Shule ya Laurent International ya Pemba baada ya mwalimu wake mmoja kudaiwa kumpiga mwanafunzi bakora na kusababisha kifo chake.

Mwalimu huyo alichukua hatua hiyo baada ya mwanafunzi kuharibu kifaa cha kuhifadhia gundi aliyoomba kwa ajili ya kuunganisha godoro lake.

Mwalimu huyo alikuwa akimchapa mwanafunzi viboko huku akimzungusha katika madarasa yote 13 ya shule hiyo, kitu kinachotia shaka mwenendo wa mwalimu huyo.

Kutokana na kitendo hicho, SMZ imefunga shule hiyo huku uchunguzi unaendelea ili kupata ushahidi wa tukio hilo na ikiwezekana kumfikisha mahakamani mwalimu aliyehusika.

Hilo ni moja ya matukio ya hivi karibuni ya walimu kuchukua hatua zinazozidi mipaka dhidi ya wanafunzi.

Ni hivi karibuni tu mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Matwinga mkoani Mbeya alituhumiwa kusababisha kifo cha mwanafunzi baada ya kuadhibiwa kwa kufungiwa ndani ya chumba kidogo cha kuhifadhia nyaraka, maarufu kama kasiki.

Mwanafunzi huyo alifungiwa pamoja na mwenzake kwa madai kuwa hawakuonekana shuleni kwa muda wa siku tano.

Mwaka jana, walimu waliokuwa mazoezini mkoani Mbeya walishirikiana kumpiga mwanafunzi wakidai kuwa alikuwa mjeuri. Picha za video ziliwaonyesha walimu hao wakimchangia mwanafunzi huyo kwa kumpiga huku wakisema maneno yanayoonekana kuwa wamepania kumkomoa.

Kwa kusoma magazeti, kuangalia televisheni na kusikiliza redio, tunapata habari nyingi za matukio ya adhabu za kikatili dhidi ya wanafunzi zinazotolewa kwa mgongo wa kurekebisha tabia sugu za wanafunzi.

Inaonekana matukio ya walimu kutoa adhabu hizo za kikatili yanayoripotiwa ni machache kuliko hali ilivyo shuleni. Inawezekana kabisa kuna adhabu kubwa zaidi wanazopewa wanafunzi, lakini haziripotiwi kwa sababu mambo hayajaharibika kama ilivyo kwa matukio tuliyoyaonyesha hapo juu.

Hii ni ishara kwamba kuna mambo hayaendi vizuri katika mafunzo ya walimu, kiasi cha kusababisha hali hiyo kutokea.

Imani yetu ni kwamba walimu wana stadi hizo za kurekebisha wanafunzi bila ya kuwa na madhara, lakini ongezeko la matukio ya adhabu ambazo zinafikia hatua ya kusababisha mauti na udhalilishaji, ni ishara kwamba kuna kitu lazima kifanyike kabla ya mambo kuwa mabaya zaidi.

Ni dhahiri, tukio la Mbeya la wanafunzi kufungiwa ndani ya kasha hilo la nyaraka lilijulikana kwa walimu wengine, lakini hawakuchukua hatua zozote za kuripoti hadi mwanafunzi alipofariki.

Na hata tukio la mwanafunzi kushambuliwa na walimu wapatao wanne lisingeweza kujulikana kama mkanda wa video usingerushwa katika mitandao ya kijamii, kama ilivyo kwa tukio la Zanzibar ambalo lilijulikana baada ya mwanafunzi kufariki.

Kwa hiyo, kuna tatizo katika mfumo wa uzalishaji walimu na pia mfumo wa kushughulikia wanafunzi wanaoonekana kuwa hawawezekani.

Mwalimu mmoja hatakiwi kujibebesha mamlaka ya mwisho kumshughulikia mwanafunzi anayeonekana ameshindikana, bali jambo hilo liwe shirikishi, yaani kuwepo na vikao na viongozi wa juu wa shule kabla ya kutaarifu wazazi.

Pia, mfumo wa kuzalisha walimu ni lazima uangaliwe kama una kasoro zinazofanya kuwe na ongezeko la vitendo vya walimu kuadhibu wanafunzi kikatili kiasi cha kufikia kupoteza maisha.

Mamlaka husika hazina budi kuliangalia ongezeko hilo la adhabu za kikatili kwa jicho la karibu zaidi na kuchukua hatua zinazostahili ili kukabiliana na madhara yanayoweza kuepukika.

0 Comments