WAZAZI JUKUMU LENU LA ELIMU KWA WATOTO WENU LIKO PALEPALE

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo wa Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.

SERIKALI imewataka wananchi kuacha upotoshaji kuhusu mpango wa Serikali kutoa elimu bure, kwamba wazazi na walezi hawatakiwi kusaidia kitu chochote katika kufanikisha masomo kwa watoto wao.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako (pichani) alisema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Loleza, lililokarabatiwa kwa Sh milioni 20 na taasisi ya Tulia Trust inayoongozwa na Naibu Spika, Tulia Akson.

Alisema kumekuwa na upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu, kuwa hivi sasa elimu ni bure, hivyo wazazi hawatakiwi kusaidia chochote kuboresha elimu na mazingira bora ya kusomea kwa wanafunzi.

Alisema Rais Dk John Magufuli, aliamua kuanzisha mpango wa elimu bure baada ya kuona Watanzania wengi hawana uwezo wa kuwalipia watoto wao ada za shule na kusababisha watoto wengine washindwe kuanza darasa la kwanza.

Profesa Ndalichako alisema serikali imefuta michango ya lazima, ikiwemo ada za shule ili kuwezesha Watanzania wa kipato cha chini kupata elimu. Hata hivyo, alisema iwe ni kwenye elimu ama afya, hakuna Mtanzania atakayezuiwa kuchangia kwa kujenga au kufanya ukarabati.

Alisema wanaofanya upotoshaji wanatakiwa kuacha ili kutowakatisha tamaa wale wenye moyo kujitolea. Alisisitiza umuhimu wa Watanzania kuunga mkono jitihada za serikali, za kuhakikisha inaleta maendeleo ambayo yataletwa na Watanzania wenyewe, pasipo kutegemea misaada kutoka nje.

0 Comments