MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma imemhukumu kifungo cha mwaka moja gerezani mwalimu wa Shule ya Msingi Mtamba iliyopo katika Kata ya Rudi, Stephano Kuchera kwa makosa ya wizi wa vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilo kumi za unga.
Kesi hiyo iliyokuwa ya rufaa kutoka katika Mahakama ya Mwanzo, Chipogolo ilitolewa hukumu juzi na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa, Pascal Mayumba. Mshitakiwa huyo ambaye alikuwa ni mwalimu wa shule ya msingi Mtamba alishitakiwa kwa kosa la kuvunja na kuiba mali kadhaa za Zena Hosea, ikiwemo redio moja, pasi ya mkaa na unga kilo 10.
Hakimu Mayumba alisema mshtakiwa huyo alifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha Sheria Namba 273 C ya Kanuni ya Adhabu Sura Namba 16. “Kwa mujibu wa kifungu hicho cha sheria ambacho kinatamka wazi kuwa kama mtu aliyepatikana na hatia na kuvunja na kuiba adhabu yake ni kifungo cha gerezani, miaka 14 kosa la kuvunja na miaka saba na kosa la kuiba miaka saba,” alisema Hakimu Mayumba.
Alipotakiwa kujitetea, mwalimu huyo aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ana majukumu ya serikali pia na familia yake ikiwemo wazazi wake na watoto wa ndugu zake ambao anawasomesha na wanamtegemea pia ni kosa lake la kwanza. Hakimu Mayumba alisema kutokana na mwenendo wa kesi mahakama inamhukumu kutumikia kifungo cha mwaka moja gerezani. Alisema kwa ambaye hataridhika na maamuzi ya mahakama anaweza kuipinga adhabu hiyo ndani ya siku 30.
0 Comments