NANI MDHIBITI WA USALAMA NA UBORA WA CHAKULA MASHULENI?



Kwa ufupi

Kimsingi, chanzo cha magonjwa hayo ya kuhara, minyoo na kichocho ni uchafu unaosababishwa na kula vyakula bila kunawa, kunywa maji yasiyochemshwa na kucheza kwenye maji yaliyotuama.

Hivi karibuni, kulikuwa na kazi ya utoaji chanjo kwa watoto wa miaka mitano hadi chini ya 15, kwa ajili ya kutibu magonjwa yasiyopewa kipaumbele.

Kimsingi, chanzo cha magonjwa hayo ya kuhara, minyoo na kichocho ni uchafu unaosababishwa na kula vyakula bila kunawa, kunywa maji yasiyochemshwa na kucheza kwenye maji yaliyotuama.

Vyanzo hivi vinaweza kuepukika ikiwa wazazi, walimu na wataalamu wa afya watatimiza wajibu wao kwa watoto na hatimaye kuwa na Taifa wenye afya njema.

Mkoa wa Kigoma unatajwa kuongoza kwa kuwa na watoto wenye matatizo mengi ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele na kufuatiwa na mikoa ya kanda ya Ziwa.

Leo ukipita maeneo ya shule za msingi, karibu kila pembe ya nchi, hutokosa kukuta wachuuzi, hasa kina mama wakiuza vyakula.

Uzoefu unaonyesha baadhi ya wamiliki wa biashara hizi ni walimu na hata wataalamu wa afya.

Lakini, mazingira ya biashara hizi si rafiki kiafya na inavyoonekana hakuna anayesimamia kujua usafi na ubora wa vyakula vinavyouzwa.

Watoto wananunua maandazi kwa mfano, hawana maji ya kunawa na hakuna vifaa vya kuhifadhia chakula hicho. Huku ni kujitakia magonjwa kwa makusudi.

Inashangaza kuona katika maeneo mengi maofisa wa afya wanajihimu kuwafungia mamantilie mitaani, lakini wanashindwa kufanya hivyo kwa wauzaji wa vyakula visivyo na sifa shuleni.

Lawama pia nazielekeza kwa walimu. Wanawafundisha watoto usafi darasani, lakini nje walimu haohao ndio wanaouza vyakula katika mazingira machafu.

Inawezekanaje walimu wakawaadhibu watoto kwa kuvaa nguo chafu, kutokata kucha, kutovaa viatu, lakini wakawaruhusu kula vyakula bila kunawa?

Haipendezi kwa wataalamu wa afya, wazazi walimu na kamati za shule kufumbia macho hali hii inayoweza kuwaathiri watoto kiafya na kitaaluma.

Nashauri kuwa ama uuzwaji wa vyakula hivi usitishwe au kuwekwe mazingira rafiki kiafya kwa wachuuzi na hata wanafunzi. Miongoni mwa mbinu ni pamoja kuwahimiza wafanyabishara kuwa na vifungashio safi na sio vipande vya magazeti au mifuko ya nailoni.

Aidha, wazazi wasiwe wepesi kutoa fedha kwa watoto wao kununua vyakula pasipo kujiridhisha ubora, usafi na usalama wa vyakula hivyo.

Wakumbuke kuwa athari ya kumnyima mtoto fedha za matumizi ni ndogo kuliko gharama za kumtibu anapokumbwa na magonjwa yanayotokana na kula vyakula visivyokuwa salama.

Wazazi hawana jinsi ya kukwepa jukumu la ulinzi na usalama wa watoto wao ikiwamo suala la afya.

Kwa wale wazazi wenye uwezo wa kuwafungashia chakula watoto wao, ni bora wakafanya hivyo kwa minajili ya kuwaepusha na magonjwa.

Nawaomba viongozi kwa ngazi zote za kiserikali kuanza sasa kuhimiza usafi katika mazingira ya shule, badala ya kushupalia shughuli za usafi za kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.

Ujenzi wa taifa unaanza kwa watoto wenye afya, tuimarishe afya kwa watoto shuleni ili iwe chachu ya kufanya vizuri kitaaluma na baadaye kuwa nguzo ya maendeleo kwa nchi yetu.

Leo tunadharau hili, kukitokea janga ndipo tuanze kuwajibishana

0 Comments