JAMII INAHITAJI ELIMU YA MADHARA YA VIPODOZI

Kwa ufupi

Mara nyingi baadhi ya watu wanaposikia neno kipodozi, mawazo yao uhamia katika vitu anavyodhani kuwa vinatumiwa zaidi na wasichana na wanawake.

Vipodozi ni bidhaa ambayo kila mara hutumiwa zaidi na wanawake kwa lengo la kuiweka miili yao katika hali ya usafi na utanashati kwa mtumiaji.

Mara nyingi baadhi ya watu wanaposikia neno kipodozi, mawazo yao uhamia katika vitu anavyodhani kuwa vinatumiwa zaidi na wasichana na wanawake.

Lakini ikumbukwe hii ni bidhaa inayoweza kutumiwa hata na mwanaume kwani lengo ni kumfanya mtu aonekane mtanashati.

Kiuhalisia, kipodozi ni pamoja na sabuni tunazotumia kila siku, mafuta ya kujipaka, manukato, mafuta, krimu na jeli ambazo hutumiwa na watu wa jinsia zote.

Maana ya kipodozi haitabadilika ingawa bidhaa hizi zipo za wanawake, watoto na wanaume na vyote huitwa vipodozi.

Hata hivyo, hivi karibuni baadhi ya wanawake wameamua kwa utashi wao kuvitumia vipodozi hivyo kwa lengo la kujichubua ngozi ili aonekane mweupe badala ya rangi yake ya asili ya weusi.

Nimeamua kuandika haya leo baada ya kushuhudia mjadala mpana uliojitokeza kwenye Tamasha la Jinsia Tanzania 2017 lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia (TGNP) kwa kushirikiana na washirika wake na kufanyika katika viunga vya ofisi zao, Mabibo jijini Dar es Salaam.

Wakizungumza katika tamasha hilo, baadhi ya wakulima kutoka mikoa tofauti nchini, walisema madhara ya vipodozi vyenye kemikali ya sumu yanawatisha.

Binafsi nilijiuliza kwanini wamesema hivyo, lakini nikajipatia jibu pia mwenyewe, huenda wameshapata elimu ya utambuzi wa athari ya matumizi ya vipodozi vyenye viambata sumu.

Kwani tangu kuanza kwa udhibiti wa vipodozi nchini, aina 250 vimegundulika kuwa na viambata sumu na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ilishapiga marufuku matumizi yake nchini wala kuingizwa kutoka nje.

Meneja na mtaalamu wa masuala ya kemikali kutoka Taasisi ya Envirocare, Euphrasia Shayo akiwasilisha mada yake kwa kundi hilo la wakulima walioshiriki tamasha hilo, kemikali za sumu za zebaki na mericuri zilizomo katika vipodozi na mikorogo isiyo rasmi inayotumiwa hasa na akinamama kujichubua na kubadili nywele zao, zina madhara makubwa pia kwenye kilimo.

Kwani kemikali hizo mbali na kukaa ardhini kwa muda mrefu zikiharibu mazao, pia zinamadhara makubwa kwenye miili ya binadamu, hivyo aliwashauri kuachana navyo mara moja kwa wale wanaoendelea kuvitumia.

Wapo ambao watajiuliza kemikali hizo zilizomo kwenye vipodozi zinauhusiano gani na mwili wa binadamu na ardhi.

Baada ya kumsikiliza kwa makini mtaalamu huyo, nilibaini kuwa kemikali hizo baada ya kutumiwa na muhusika, makasha yake hutelekezwa ardhini na mvua zikinyesha husafirishwa hadi kwenye vyanzo mbalimbali vya maji, hivyo kujikuta maji hayo yakitumiwa tena na binadamu, jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya watu na mifugo.

Lazima tukubali na kuanza kuchukua hatua kuepukana na kadhia hii. Tumeshaambiwa na wataalamu vinamadhara makubwa kwa miili yetu, ndiyo maana sasa hivi magonjwa ya ajabu ajabu yakiwamo ya kansa yameendelea kushamiri.

Wapo wanawake wengi walioathiriwa kwa kiwango kikubwa na kemikali hizo zenye sumu.

Baadhi ya wakulima washiriki katika mjadala huo waliiomba Serikali kuwatumia wataalamu kutoa elimu ya madhara kupitia vyombo vya habari vya redio, luninga na magazeti ili kila mmoja aelewe madhara ya vipodozi hivyo.

Ukitazama kwa kina, ombi la wakulima hao lina mashiko, kwani muarobaini wa matatizo mengi yanayowakumba watu wengi ni elimu.

Ukosefu wa elimu ya kina kwa kila jambo huzua madhara makubwa kwa jamii inaweza kuwa saa au hata baadaye.

Kwa mfano tunapozungumzia matumizi ya vipodozi, watu waishio vijijini wengi hawaelewi kama kuna vyenye viambata sumu.

Wanajua vipodozi vyote viko salama ndiyo maana wenzao wanaovitumia wanapendeza na kuonekana kuwa wenye mvuto mbele za watu.

Ndiyo maana nao hutamani waonekane watanashati kama wenzao waishio mijini.

Hivyo ili kufikia lengo hilo, huamua kutumia kila kipodozi watakachoambiwa kinafaa bila kukifanyia uchunguzi au utambuzi wa kiafya wa ngozi.

Vipodozi vyenye viambata sumu vipo vingi, lakini kama mtu hataweza kuvitambua au kuelimishwa anajikuta ametumbukia kwenye matumizi yake yasiyo salama.

Ili kuwanusuru hususan wanawake na wasichana Wakitanzania wasiendelee kudhurika na vipodozi hivyo, Serikali, asasi zisizo za kiserikali na taasisi kama Envirocare, watumie mbinu mbalimbali kufikisha elimu hii ya vipodozi salama kwa jamii bila kuangalia maeneo.

Matamasha kama hili la Jinsia, pia ni mahali muafaka pa kufikisha ujumbe kwani watu kutoka maeneo mbalimbali nchini hukusanyika kujifunza mambo kadha wa kadha.

Lakini pia waelimishaji hawa sasa waone umuhimu wa kupeleka elimu hiyo kwenye maeneo ya pembezoni.

Lakini pia oparesheni za kuwakamata na kuwachukulia hatua kali waingizaji wa vipodozi vyenye viambata vya sumu zisifanywe kwa mtindo wa zima moto, bali ziwe endelevu

0 Comments