HUU NI UFUMBUZI WA TAKWIMU MASHULENI

Mkurugenzi Mkuu Kampuni ya Eagle Analytics, Rose Funja ambao ni wasimamizi wa mfumo huo akifafanua machache mbele ya wanahabari jijini Dar es Salaam jinsi mfumo huo unavyofanyakazi. Pembeni ni Meneja Ufuatiliaji na Tathimini mradi wa Data kwa Maendeleo ya Jamii wa Tume ya Sayansi na Teknolojia, Dk. Geofrey Chambua.

MFUMO mpya wa kieletroniki wa ‘Dopwall’ umezinduliwa nchini na unatajwa kuwa utasaidia kupunguza mdondoko wa elimu kwa wananchi wa kike nchini.

Licha ya hali hiyo pia inatajwa kuwa mdondoko wa wanafunzi kwa shule bado ni tatizo nchini ambapo kwa kipindi cha mwaka 2015 wanafunzi 61,488 waliripotiwa kuacha masomo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi Mkurugenzi Mkuu Kampuni ya Eagle Analytics, Rose Funja, alisema kuzinduliwa kwa mfumo huo kusaidia wazazi na walezi kujua hali ya maendeleo ya shule wanasoma watoto wao ikiwemo kuwa na uwezo wa kuhoji kupitia vikao vya wazazi na bodi za shule.

“Serikali kupitia wizara mbalimbali ikiwemo Serikali za Mitaa wameboresha ukusanyaji wa taarifa mbalimbali za kielimu ambazo ni msingi wa mapambano dhidi ya mdondoko wa wanafunzi. Pamoja na jitihada hizo matumizi ya taarifa kama hizo katika kuboresha utendaji wa kila siku wa watumishi wa umma na ufanyaji wa maamuzi hayatoshelezi au hakuna kabisa katika idara za serikali,” alisema Funja

Kwa upande wake Meneja Ufuatiliaji na Tathimini mradi wa Data kwa Maendeleo ya Jamii wa Tume ya Sayansi na Teknolojia, Dk. Geofrey Chambua, alisema mfumo wa kieletroniki wa ‘Dropwall’ unalenga kuongeza matumizi ya taarifa zinazokusanywa na wadau mbalimbali ikiwemo serikali.

“Ubunifu wa mfumo huu umedhaminiwa na mradi wa Data fot Local Impact (DLI) ikiwa ni moja kati ya miradi mitatu ya takwimu inayosimamiwa na MCC pamoja na PEPFAR. Udhamini wa dli uliwesha uchunguzi wa mdondoko mashuleni katika wilaya za Mbeya na Nzega chini ya mwongozo wa TAMISEMI.

“Kampuni ya Eagle Analytics inayotengeneza mfumo wa Dropwall ni kampuni changa. Mhandisi Rose na timu yake kupitia ubunifu wao wa kubaini uwezekano wa mwanafunzi kuacha masomoni mmoja wa washindi 12 wa shindano la ubunifu lililoratibiwa na DLI ikishirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) mwaka 2016,” alisema Dk. Chambua

0 Comments