CHUO KIKUU CHA KENYATTA CHAFUNGWA


Kwa ufupi

Walidai kwamba timu hiyo ya uongozi “ilitangulizwa” na “ikadhaminiwa” na menejimenti ya chuo na kwa hiyo haifai kuwakilisha masilahi ya wanafunzi wengine.

Nairobi, Kenya. Chuo Kikuu cha Kenyatta kimefungwa kwa muda usiojulikana na wanafunzi wameamriwa kuondoka mara moja.

Kufungwa kwa chuo hicho kumetokana na ghasia za usiku kucha zilizofanywa katika kampasi kuu ambako wanafunzi walichoma jengo la zamani la utawala, kwa madai kwamba wanapinga uongozi mpya wa wanafunzi uliochaguliwa.

Kwa mujibu wa wanafunzi waliozungumza na Nation Ijumaa, mgomo uliandaliwa kuelezea kutoridhishwa kwao na uongozi mpya wa wanafunzi Kenya University Students Union (Kusu) ambao ulichaguliwa Jumanne.

Walidai kwamba timu hiyo ya uongozi “ilitangulizwa” na “ikadhaminiwa” na menejimenti ya chuo na kwa hiyo haifai kuwakilisha masilahi ya wanafunzi wengine.

"Vilevile hatukuwa tunataka kufanya mitihani iliyopangwa kuanza Jumatatu ya wiki ijayo kwa sababu tulijiona hatukuwa tayari kwa sababu wahadhiri wengi hawakuwepo kwa muda mrefu kutokana na mgomo wao,” alisema mwanafunzi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Walisema muhula wa masomo ulivurugwa na mgomo wa wahadhiri. "Hatukuwa tumesoma kiwango cha kufanya mitihani. Baadhi ya wanafunzi walikwisharudi nyumbani baada ya kujulikana wahadhiri walikuwa kwenye mgomo. Walikosa hata kufanyiwa tathmini ya majaribio," waliongeza.

Lakini mwanafunzi mwingine aliyezungumza na Nation alisema hakuwa anajua sababu hasa za mgomo huo.

Soma: Raila atua Nairobi, polisi wakifukuza wafuasi wake

"Nilikuwa nimekwenda nyumbani baada ya matokeo kutangazwa kwa sababu tulikuwa tumechoka sana. Baadaye nilisikia wanafunzi wanaandamana. Siwezi kusema kwa nini."

Wanafunzi walioko katika mgomo wametoa kile walichokiita “masharti yasiyopunguzika”ambayo wanataka menejimenti itekeleze.

Masharti hayo ni kwamba wanataka menejimenti ya chuo ifumuliwe, yafanyike marekebisho ya Sheria ya Chuo Kikuu ya mwaka 2016 ili kuiondoa ‘tume ya uchaguzi wa wanafunzi’, sera za chuo zipitiwe upya, mchakato wa nidhamu ya wanafunzi, kuondolewa kwa ada ya ziada na mengineyo.

0 Comments