Kwa ufupi
Kikao kimeitishwa kujadili hali iliyotokea kisiwani Soswa baada ya walimu kukutwa wamelala nje
Buchosa. Siku moja baada ya walimu saba wa Shule ya Msingi Soswa kujikuta wamelala nje na kati yao wawili kunyolewa nywele kichwani na sehemu za siri, uongozi wa kisiwa cha Soswa umeitisha mkutano wa hadhara kujadili suala hilo.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Soswa, Rafael Majura amesema mkutano huo utafanyika leo Alhamisi katika kisiwa hicho ambapo utahudhuriwa na wazee maarufu na viongozi wa Kata ya Bulyaheke.
Amesema mkutano huo utajadili namna ya kukabiliana na tukio hilo ambalo limeleta taswira mbaya kwenye jamii na Taifa kwa ujumla.
“Tunategemea kuanza mkutano wa hadhara ili kujadilia suala hili ambalo limechafua taswira ya kisiwa hiki na kuleta hofu miongoni mwa walimu,” amesema Majura
Majura amesema tayari viongozi wa kata hiyo wakiongozwa na Mtendaji wa Kata ya Bulyaheke, Musa Mwilomba wamekwisha fika kwa ajili ya kikao hicho.
Mkazi wa kisiwa hicho, Mjura Magafu amesema kitendo hicho kimeleta aibu kubwa na kwamba ni lazima waliofanya wapatikane na waadhibiwe.
“Na ikiwezekana tutapiga kura kuwabaini watu hao waliochafua taswira ya kisiwa chetu,” amesema Magafu.
0 Comments