RWANDA KUKUZA LUGHA YA KISWAHILI KWA VITENDO

KWA sasa nchi nyingi duniani, zinafurahia lugha ya Kiswahili na hata kukifundisha katika ngazi mbalimbali za elimu, ikiwemo vyuo vikuu.

Baadhi ya nchi ambazo tayari zimechukua hatua za makusudi kutumia Kiswahili ni Ujerumani, Urusi, China, Korea Kusini, Japan na Marekani. Hivyo, kutokana na umuhimu huo, tunapongeza tukio kubwa la mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), ilizindua rasmi usambazaji na uuzaji wa toleo maalumu la Afrika Mashariki la gazeti la HabariLeo nchini Rwanda.

Uzinduzi huo ulifanywa na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Ali Idi Siwa na kuhudhuriwa na baadhi ya wananchi wa Rwanda, wakiwemo wasomi na wataalamu wa Kiswahili, wanafunzi wa vyuo vikuu na Watanzania waishio Rwanda, ambapo Balozi Siwa aliwataka waliohudhuria hafla hiyo kuwa mabalozi wazuri.

Pia, tunapongeza hatua hiyo, kwa sababu gazeti hili litazidi kukuza na kuendeleza Kiswahili na kuimarisha Mtangamano wa Afrika Mashariki katika nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Nchi nyingine wanachama wa jumuiya hiyo ni Tanzania, Kenya, Burundi, Uganda na Sudan Kusini.

Ni wazi kuwa uzinduzi huo wa gazeti hili nchini Rwanda, unaunga mkono mikakati ya Serikali ya Rwanda ya kuiimarisha lugha hiyo, ambapo hivi karibuni iliamua kulifanya somo la Kiswahili kuwa la lazima kwa wanafunzi wa sekondari.

Tayari Bodi ya Elimu Rwanda (REB) imezindua matumizi ya mtaala mpya, utakaowalazimisha wanafunzi katika shule za sekondari kujifunza Kiswahili na watafanya mtihani wa taifa wa somo hilo kuanzia mwakani.

Mtaala huo utakaozingatia uwezo wa wanafunzi, una lengo la kuwezesha nchi hiyo kupata maendeleo endelevu na kuwa na uhakika wa ubora wa elimu. Aidha, tunaunga mkono kauli ya hivi karibuni ya Naibu Waziri Mkuu wa Pili wa Uganda anayeshughulikia Masuala ya EAC, Kirunda Kivejinja aliyesisitiza umuhimu wa wananchi wa nchi za EAC, kutumia Kiswahili ili kuwaunganisha.

Kivejinja ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri EAC anasema nchi wanachama wa EAC, hazitafanikiwa kutekeleza Kifungu cha 137 (2) cha Makubaliano ya kuanzishwa jumuiya hiyo, kama hazitatumia Kiswahili.

Anasema ni muhimu Kiswahili kifanywe rahisi na watu wengi wakitumie sanjari na lugha zao za asili. Hali kadhalika, tunasisitiza ahadi aliyotoa Mhariri Mtendaji wake, Dk Jim Yonazi, kwenye uzinduzi huo huko Rwanda, ambapo aliwaahidi wananchi wa Rwanda kwamba TSN itawaongoza katika safari ya kukuza na kuendeleza Kiswahili kupitia gazeti la HabariLeo.

Kwa hakika, gazeti hili litakuwa daraja la kukivusha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya EAC na litawaunganisha kirahisi wananchi zaidi ya milioni 150 wa Afrika Mashariki

0 Comments