AGIZO ELIMU BURE LAIBUA CHANGAMOTO

Kwa Ufupi

Wazazi Tabora wagawana mchele waliochangia shuleni baada ya Rais kupiga marufuku michango.

Dar/Mikoani. Wakati suala la chakula likionekana kuwa tatizo kubwa katika utekelezaji wa agizo la kufuta michango, wazazi 123 mjini Tabora wamegawana fedha walizokuwa wamechangia kwa ajili ya huduma za shule na wanafunzi.

Utoaji wa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, ni moja kati ya mambo yaliyo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na Rais John Magufuli ameanza kuitekeleza kwa kupiga marufuku michango ya aina yoyote shuleni.

Kama haitoshi, Rais alirudia agizo lake Januari 17 alipotoa onyo kuwa endapo atasikia tena wazazi wakilalamikia michango, mkurugenzi wa wilaya husika ajifute kazi.

Serikali inatoa Sh23.8bilioni kila mwezi kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa elimu bila malipo, lakini utekelezaji wa agizo hilo unakosolewa kutokana na umuhimu wa chakula kwa shule za kutwa, hasa kutokana na ukweli kuwa baadhi ya wanafunzi wanaishi mbali na shule

Uzoefu unaonyesha katika shule za nje ya miji, wanafunzi hutakiwa kufika saa 1:30 asubuhi ili kuanza masomo saa 2:00 asubuhi na hupumzika mchana kwa ajili ya chakula, lakini sasa inabidi vipindi viishe saa 8:30 mchana.

“Dhamira ya Rais ni njema, lakini fedha inayopelekwa haiwezi kutosheleza mahitaji yote,” alisema aliyekuwa ofisa elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mapunda.

“Kwa mfano nakumbuka kuna shule moja pale Buguruni ilikuwa na wanafunzi 124 na ilipokea Sh67,000 tu ambazo hazikutosheleza. Suala la ulinzi, umeme na chakula ni changamoto katika shule nyingi.

“Serikali ikiunganisha huduma hizo kwa kuongeza bajeti, michango haitakuwa na ulazima.”

Changamoto ni chakula

Alisema athari zinazoweza kujitokeza endapo michango yote itafutwa ni pamoja na wanafunzi wengi kutofanya vizuri katika masomo yao kutokana na ukosefu wa chakula.

Maoni kama hayo yalitolewa na Profesa Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye alielezea umuhimu wa walimu kushiriki kikamilifu katika elimu ya watoto wao, kama kutoa michango ya msingi ya chakula, maji, ulinzi hata ujenzi wa miundombinu.

Profesa Bana alisema wazazi wakisitisha kuchanga kwa sababu ya agizo la elimu bila malipo, kunaweza kukawa na madhara kwa sababu ni ukweli usiopingika kwamba afya ya mwili huenda sambamba na afya nzuri ya mwili.

“Kwa uzoefu wangu wa kufundisha shule za msingi, lazima elimu iwe shirikishi kwa maana ya wazazi kuchangia ni vigumu kumuelewesha mtoto aliye na njaa,” alisema Profesa Bana.

“Wanaomshauri Rais Magufuli waangalie masuala ya msingi yanayoweza kuchangiwa na wazazi, hasa chakula shuleni.”

Alisema msingi wa elimu ya kujitegemea lazima uende sambamba na jamii husika kuchangia elimu bila wasiwasi.

“Kama walimu wanahofiwa kupokea michango, kamati za shule ziunde kamati ndogo za kupokea michango ili huduma muhimu kwa watoto ziendelee. Huwezi kuacha watoto na njaa wakati wazazi walikuwa wanachangia na wana uwezo huo,” alisisitiza.

Mtaalamu mwingine aliyezungumzia suala hilo ni mratibu wa Mradi wa Mtoto Mwerevu kutoka Jukwaa la Lishe Tanzania (Panita), Ruth Maziku aliyesema ipo hatari ya kushuka kwa kiwango cha elimu iwapo wanafunzi hawatapata chakula.

Alisema katika umri wa miaka mitano hadi 14 ambao mwanafunzi anatarajia awe kati ya darasa la kwanza na la saba, chakula ndio msingi mkubwa wa kukuza ufaulu.

“Kwa umri huo anapaswa kula milo mitano, mitatu ikiwa mikubwa na miwili midogo. Chakula kinasaidia ubongo kufanya kazi yake ipasavyo na kuongeza uelewa kwenye masomo,” alisema.

Mtaalamu huyo alisema ukosefu wa chakula unaweza kuongeza utoro kwa wanafunzi wanaoishi mbali na shule.

“Kwa hiyo wataalamu wa lishe tunasisitiza watoto kupata chakula cha mchana shuleni,” alisema.

Viongozi wa mikoa, wilaya wanena

Mkoani Iringa, mkuu wa mkoa, Amina Masenza alisema Serikali haijapiga marufuku michango ya wazazi kwa ajili ya maendeleo ya shule, bali inayokusanywa na walimu.

Masenza alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika kata za Nyanzwa na Ibumu Wilaya ya Kilolo.

“Ni marufuku michango yote inayotolewa na wanafunzi kwa walimu. Mwalimu atakayebainika kuhusika na hatua kali zitachukuliwa dhidi yake. Wanafunzi wanatakiwa kupokewa shuleni na kuendelea na masomo bila ya kusumbuliwa,” alisema Masenza.

“Kama wananchi mtakaa wenyewe na kukubaliana kuwa mnachanga kwa ajili ya maendeleo ya shule zenu bila ya kuhusisha mwalimu katika michango hiyo, hapo mnaruhusiwa. Hata waraka wa elimu bila malipo unasema hivyo.”

Masenza alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa maswali na baadhi ya wakazi wa Kata ya Ibumu waliotaka kujua aina ya michango iliyopigwa marufuku na ile inayoruhusiwa.

Katika majibu yake, alisema michango inayoibuliwa na jamii haina budi kusimamiwa na jamii husika bila kuwahusisha walimu, kuanzia ukusanyaji wa michango hadi matumizi yake.

Kuhusu malipo ya walinzi, mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli alisema suala la ulinzi wa shule, halmashauri yake inalipa mishahara yao katika shule zote za wilaya hiyo.

“Kuhusu usafi huo ni wajibu wa wanafunzi, na chakula tunatoa kwa wanafunzi wa bweni tu, chakula cha nini kwa mwanafunzi wa kutwa,” alihoji.

Naye katibu tawala wa Wilaya ya Kilombero, Robert Selasela alisema utaratibu wa michango ya ulinzi na chakula vinatekelezwa katika serikali ya kijiji.

Kuhusu mwongozo wa elimu bila malipo, Selasela alisema licha ya maelekezo ya fedha kujikita katika vifaa vya ufundishaji, ukarabati wa shule, huduma za kiutawala na mengineyo, bado wanavijiji wameamua kuchangia mahitaji ya chakula bila kushirikisha uongozi wa shule.

“Shule ni mali ya serikali ya kijiji. Rais anatukumbusha tu, ruzuku tuliyopata hadi Novemba mwaka jana ilikuwa ni Sh285.9 milioni, sawa na asilimia 73 ya Sh440 milioni. Bajeti ni Sh20,000 kwa kila mwanafunzi,” alisema.

“Kuhusu michango ya chakula ni wanakijiji wanakusanya chakula, si pesa na wanatumia kamati zao na kupika wenyewe.”

Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Zuwena Omary alisema licha ya michango kupigwa marufuku, jamii inapaswa kutambua majukumu ya wazazi na Serikali katika suala la elimu bure.

Alisema suala la wazazi na walezi kuchangia shule za msingi na sekondari za kata ambazo wanafunzi wanaishi kwenye hosteli halikwepeki.

Wazazi walivyogawana michango

Mkoani Tabora wazazi 123 wa watoto wanaosoma Shule ya Msingi Ipuli , wamegawana fedha taslimu na vyakula walivyonunua kwa ajili ya mlo wa mchana, ikiwa ni kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais la kuzuia michango shuleni.

Makamu mwenyekiti wa kamati ya wazazi wa shule hiyo, Samson Gabriel alisema uamuzi wa kuwarejeshea wazazi hao michango hiyo ya chakula na fedha ni utekelezaji wa agizo la Rais na maelekezo ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.

Kwa mujibu wa mwalimu mkuu wa shule hiyo, Mariam Hamis wazazi hao walichanga Sh676,000 mpaka kufikia Januari 17 na Sh272,000 zilikuwa zimetumika kununua mahindi na mchele.

“Baada ya agizo la Serikali, wazazi wameamua kugawana Sh404,000 zilizosalia pamoja na chakula kilichokuwa kimenunuliwa ambacho ni mahindi na mchele,” alisema Mariam.

Mmoja wa wazazi walioshiriki kugawana fedha na vyakula hivyo, Perpetua Kamiliwe , ambaye alikuwa ameshika kiroba cha mchele, alisema mambo yalikuwa mazuri.

“Nimechukua mchele wenye thamani ya pesa niliyochangia. Sioni kama kuna jambo limeharibika,” alisema.

Mzazi mwingine, Ibrahim Zuberi aliliambia Mwananchi kuwa licha ya kugawana chakula hicho, wanaishukuru Serikali kwa kupiga marufuku michango katika shule za umma, kwa maelezo kuwa umewapunguzia wazazi gharama na ugumu wa maisha.

“Michango hii imekuwa kero na mzigo kwa wazazi tunamshukuru Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa busara. Hakika huyu ndiye kiongozi anayewajali wanyonge,” alisema.

“Michango ilikuwa ya viwango tofauti kati ya Sh6,000 hadi Sh10,000 kwa kila mwanafunzi.”

Hata hivyo, mmoja wanafunzi wa shule hiyo, Salome Yohana alisema uamuzi wa wazazi kutochangishana fedha kwa ajili ya chakula, utawaathiri katika masomo.

Imeandikwa na Robert Kakwesi (Tabora), Geofrey Nyang’oro (Iringa), Kelvin Matandiko na Tumaini Msowoya (Dar)     

0 Comments