MATOKEO DARASA LA SABA YASABABISHA WALIMU KUSHUSHWA VYEO, MANYARA.

WALIMU wakuu 28 na waratibu wa elimu kata 10 wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara wameshushwa vyeo kwa kushindwa kufaulisha wanafunzi wa darasa la saba.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hamisi Malinga alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya baadhi ya wakuu wa shule kushindwa kufikisha wastani wa kufaulisha kulingana na idadi ya wanafunzi walionao kwa asilimia 50, ikiwa ni mkakati waliojiwekea.

Alifafanua kuna walimu wakuu ambao wameshushwa vyeo kutokana na uzembe, na wengine kutokana na kukosa sifa za kuwa na elimu ya shahada ya kwanza na kwamba walimu hao watarudishwa katika nafasi zao ufundishaji.

“Walimu hao tumewavua madaraka kwa sababu wao walikuwepo tangu mwanzo na mikakati yote tuliyokuwa tumeiweka ya kimkoa, kiwilaya na kihalmashauri, tumekaa nao na tumeweka mikakati ya pamoja lakini wameshindwa kutekeleza.” Kuhusu waratibu elimu kata alifafanua kuwa hawakuwa wabunifu katika kuhakikisha kuwa elimu kwenye kata zao zinapanda badala yake baadhi yao wamekuwa wakijikita zaidi katika mambo yao ya kilimo au biashara.

Vilevile halmashauri hiyo imevunja kamati zote 28 za shule ya msingi zilizofeli na kuzitaka kuunda kamati mpya itakayoweza kusimamia mwenendo wa walimu wanafunzi na wazazi. Kwa upande wake Kaimu Ofisa Elimu Idara ya Elimu ya Msingi wa Halmashauri hiyo, Julius Sikay alisema waratibu elimu kata walioondolewa kwenye nafasi zao kutokana na ufaulu kuwa chini ya asilimia 50 ni mratibu kata ya Madunga, Boay na Dabil.

0 Comments