MVUA YAZUIA UDAHILI WA WANAFUNZI - DAR

Kwa ufupi

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kinondoni Emmanueli Kalalu amesema mvua zimeathiri upokeaji  na kuhakiki wanafunzi kutokana na hali ya hewa.

Dar es salaam. Mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam zimeathiri  upokeaji na uhakiki wanafunzi wa darasa la kwanza kutokana na idadi ndogo ya wazazi kujitokeza kuwapeleka shuleni.

Akiongea na Mwananchi leo Jumatatu  Januari 8 mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kinondoni Emmanueli Kalalu amesema mvua zimeathiri upokeaji  na kuhakiki wanafunzi kutokana na hali ya hewa.

"Kwa mwaka huu tumeandikisha wanafunzi 130 hadi muda huu saa 3 wameshafika wazazi wasiozidi 40 ndio wameleta watoto" amesema Kalalu

Amesema mwitikio kwa mwaka huu kwenye shule yake ni mkubwa tofauti na mwaka jana aliandikisha wanafunzi 101 hivyo mwaka huu idadi imeongezeka.

Kuhusu mazingira ya shule kuzungukwa na maji amesema tatizo hilo ni toka miaka ya 90 hivyo mamlaka husika inalifahamu tatizo hilo hawezi kujua sababu gani hawalitatui.

Moja ya mzazi aliyemleta mtoto wake huku akitoa sharti la kutokutajwa jina lake  amesema  tatizo hilo linawaathiri  watoto ikiwa ni pamoja na kupata fangasi miguuni kipindi cha mvua.

"Tulishauambia uongozi wa shule hata kama ni kuchangia tuchangie ili maji yanayotuama yaondoke lakini nashangaa uongozi umekaa kimya mpaka leo’’ amesema

0 Comments