TANZANIA imetunukiwa tuzo ya kimataifa, kwa kufanya vizuri katika utekelezaji wa sera za mapambano dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kupitia taasisi za kiraia.
Tuzo hiyo iliyotolewa kwa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza Tanzania (Tancda), imetolewa na Shirikisho la Kimataifa la Magonjwa Yasiyo ya Kuambukizaa kwa kushirikiana na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) za mji wa Sharjah.
Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Sarah Maongezi, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa tuzo ilitolewa Desemba mwaka jana kutokana na nchi kupitia Tancda kuweka mfumo mzuri wa uelimishaji wa jamii juu ya ufahamu wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza kupitia vyombo vya habari.
Katika mkutano huo wa jana wa kutambulisha tuzo kwa waandishi, Dk Maongezi alisema pongezi zinapaswa kutolewa kwa serikali na pia kwa vyombo vya habari mbalimbali nchini, kwa kutoa ushirikiano wa kuelimisha jamii juu ya magonjwa haya.
Alisema kwa upande wa serikali, imeweka sera nzuri juu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kuruhusu asasi za kiraia kuendesha kazi zake na hata kuzipa ushirikiano. Dk Maongezi alivitaka vyombo vya habari kupitia Chama cha Waandishi Wanaopambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TJNCDAF), kuendelea na mapambano dhidi ya magonjwa hayo kwa kupanua wigo wa uelimishaji hadi vijijini.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kati ya vifo vinavyotokea nchini, asilimia 27 inatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Kwa upande wake, mwasisi wa Tancda na Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ugonjwa wa Kisukari (TDA), Profesa Andrew Swai alisema sanjari na tuzo, walipewa dola za Marekani 5,000 ambazo wamelenga kuzitumia kufundisha walimu walioko vyuoni juu ya magonjwa yasiyoambukiza ili baada ya kuhitimu, wasaidie kuelimisha watoto shuleni.
Tuzo iliyotolewa kwa Tanzania ni miongoni mwa nyingine nne, zilizotolewa kwenye mkutano uliofanyika mjini Sharjah, UAE ambao nchi 68 zilishiriki kupitia wawakilishi wao wapatao 350 kutoka asasi mbalimbali za kiraia, zinazofanya kazi katika nchi hizo. Tancda ilishinda katika elimu kwa jamii juu ya ufahamu kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
0 Comments