UDSM YADAI KUTORIDHISHWA NA UWEKEZAJI WA MLIMANI CITY.


CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimedai kutoridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Mlimani City, unaoendeshwa na Kampuni ya Mlimani City Holdings LTD iliyo chini ya Kampuni ya A Turnstar Holdings Group ya Botswana.

Kauli hiyo ilitolewa jana kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ambayo hata hivyo iliagiza watendaji wa chuo hicho, waliosaini na mwekezaji huyo mwaka 2004 kwenda Dodoma kwa mahojiano zaidi.

Hatua hiyo ilifikiwa ikiwa ni baada ya kikao cha saa tano, kati ya wajumbe wa kamati hiyo na uongozi wa sasa wa chuo hicho. Walianza kwa kukagua eneo la miradi na kisha majadiliano. Moja ya upungufu ambao kamati hiyo ilibaini ni ucheleweshaji wa ujenzi wa hoteli ya nyota tatu katika eneo la mradi na utengenezwaji wa bustani ya kisasa, itakayokuwa na wanyama wa aina mbalimbali.

Lakini, kitu kilichowatia hasira zaidi wajumbe wa kamati hiyo ni mradi huo kutokinufaisha chuo hicho, huku mwekezaji huyo aliyeingia nchini mwaka 2004 akiwa na mtaji wa Dola za Marekani 75 sawa na Sh 150,000, akilalamika kuwa hapati faida.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka (pichani), pamoja na wajumbe wake walihamaki baada ya kubainisha udhaifu kwenye mkataba huo, ambapo Mbunge Catherine Ruge wa Viti Maalumu (Chadema) alishangazwa kwa Chuo Kikuu hicho, kumpatia mradi mkubwa mwekezaji mwenye kiasi hicho cha fedha, ambapo hata hapa nchini walikuwapo wawekezaji, ambao wangeweza kuwekeza.

Alisema, ni dhahiri kulikuwa na ubabaishaji huku akishangazwa na mwekezaji huyo, kulalamika hapati faida kwenye mradi huku akidai kuwa amechukua mkopo benki kuuendesha. Alisema, mwekezaji huyo atakuwa amewekeza kwa fedha zake na kusingizia kuchukua mkopo ili kututumia kama kigezo cha kushindwa kupata faida kwa kuwa anarejesha fedha benki, lakini pia alishangazwa kuchelewa kwa ujenzi wa bustani na hoteli kwenye eneo linalodaiwa kuwa ni la mita za mraba 40,000 ilhali wameoneshwa eneo dogo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Kaboyoka alikasirishwa kwa kutotekelezwa kwa ujenzi wa hoteli hiyo ya nyota tatu tangu mwaka 2007, iliyotakiwa kuwa na ghorofa 10 na vyumba 1000, lakini uongozi wa Mlimani City umesema utaijenga kwa kipindi cha mwaka mmoja tu. Kutokana na mazingira hayo tata, kamati yake iliagiza waliosaini mkataba huo kwenda mbele ya kamati yake bungeni. Pia, kamati hiyo iliagiza kufanyika kwa ukaguzi wa hesabu ili kubainisha deni, ambalo chuo hicho kinadai mradi huo wa Mlimani hadi sasa.

Awali akisoma ripoti ya mkataba huo, Mkurugenzi wa Mipango, Maendeleo na Uwekezaji wa Chuo Kikuu hicho, Pancras Bujulu alisema kuwa kwa miaka 10 ya kuanza kwa mradi, mwekezaji huyo amepata Sh bilioni 16 huku chuo hicho kikidai Dola 340,000, fedha ambazo PAC imeona kuwa ni ndogo na kuagiza ufuatiliaji zaidi ili kubaini deni halisi. Bujulu alisema kuwa chuo hakijapewa haki stahili ya kufuatilia pato halisi, linalopatikana kwenye mradi huo, kitu ambacho pia kiliwaudhi wabunge hao. Akitoa msimamo wa chuo kwenye kamati hiyo, Profesa Anangisye alikiri kuwepo kwa upungufu mkubwa kwenye mkataba huo na kuahidi kutoa ushirikiano stahiki kwa kamati hiyo.

0 Comments