WASICHANA WANG'ARA MITIHANI NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI


WANAFUNZI wa kike katika nchi za Tanzania, Rwanda na Kenya, wamethibitisha kuwa wana uwezo mkubwa darasani, kwa kufanya vizuri kitaifa kwenye mitihani ya kumaliza elimu ya msingi, darasa la nne, kidato cha pili na ya kuhitimu sekondari.

Katika matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya sekondari nchini Rwanda, wasichana wanne wamo kati ya watahiniwa watano bora kitaifa. Si hivyo tu, watahiniwa sita kati ya 10 bora ni wasichana.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangaza hivi karibuni na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Elimu ya Msingi na Sekondari, Isaac Munyakazi, mvulana Josyln Karenzi Manzi, kutoka Shule ya Wazazi Kigali Parents ni mtahiniwa bora kitaifa.

“Mwaka huu Bodi ya Elimu Rwanda (REB) imefanya juhudi kubwa kuongeza ufanisi. Tunatoa haya matokeo takribani wiki mbili kabla ya kuanza mwaka wa masomo, Januari 22, na hii itawasaidia wazazi kuwaandaaa watoto kwa ajili ya shule,” alisema Waziri Munyakazi.

Watahiniwa 96,595 walifanya mtihani wa taifa kidato cha nne mwaka jana nchini humo, wakiwemo wasichana 51,317 na wavulana 45,278. Watahiniwa 10 bora kitaifa kwenye mtihani huo ni Josyln Karenzi Manzi, Audry Umurerwa Gatera, Allen Kayesu, Divine Aimee Irakoze, Marie Jeanne Gentille Usanase, Theogene Twagirimana, Abdulkarim Mugisha, Ornella Irakoze Ndatabaye, Adrien Ndizeye na Anaise Marie Reginal.

Waziri Munyakazi alisema takribani asilimia 89.9 ya watahiniwa, waliofanya mtihani huo wamefaulu. Matokeo hayo yanaonesha kuwa kwenye kila somo, mtahiniwa bora kitaifa ni msichana.

“Kwenye historia ni mara ya kwanza kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi bora kutoka vijijini. Hii ilitokea kwa sababu walipewa walimu wazuri na vifaa vingine vya shule ambavyo hawakuwa navyo,” alisema.

Wavulana wamewashinda wasichana kwa idadi ya waliofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza (asilimia 61.9). Watahiniwa 10,758 ambao ni sawa na asilimia 11.14 wamefaulu kwa kupata daraja la kwanza.

Asilimia 88 ya wasichana waliofanya mtihani huo wamefaulu, na asilimia 91 ya wavulana na wamefanya vizuri. Katika matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kuhusu upimaji wa kitaifa kwa wanafunzi wa kidato cha pili na darasa la nne, wasichana waling’ara.

Kwa kidato cha pili, wasichana walishika nafasi zote 10 bora kutoka kwenye shule tatu za Feza Girls, Canossa na Precious Blood. Kwa darasa la nne, wasichana wameshika nafasi nane za juu na wavulana wakishika nafasi ya tisa na 10.

0 Comments