Mkuu wa chuo cha Aga Khan Profesa Joe Lugalla
Kwa ufupi
Pongezi hizo zimetolewa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Eleuther Mwageni wakati wa mahafali ya 13 ya chuo hicho kinachotoa kozi mbalimbali ikiwamo ya ukunga na uuguzi.
Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), kimepongezwa kwa namna kinavyotoa elimu inayosaidia kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha maisha ya raia wake.
Pongezi hizo zimetolewa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Eleuther Mwageni wakati wa mahafali ya 13 ya chuo hicho kinachotoa kozi mbalimbali ikiwamo ya ukunga na uuguzi.
Amesema elimu ni ufunguo wa maisha na kwamba Chuo Kikuu cha Aga Khan wanafanya jambo jema la kusomesha Watanzania na Serikali pekee yake isingeweza.
“Nashukuru sana Aga Khan kwa msaada huu, nyie wenyewe ni mashahidi baadhi ya wahitimu wametoka katika hospitali mbalimbali. Mbali na hili chuo hiki kimekuwa mstari wa mbele kuendeleza tafiti mbalimbali,” amesema Profesa Mwageni.
Profesa Mwageni ambaye aliwahi kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), alitumia nafasi hiyo kuwaasa wahitimu hao kuwa mabalozi wazuri pindi watakapokuwa wanatekeleza majukumu yao.
"Kumbukeni chochote mtakachokuwa mkikifanya kiwe kizuri au kibaya kitakuwa na uhusiano na AKU. Nendeni mkasaidie jamii kwa ujuzi mlioupata hapa chuoni," alisema Profesa Mwageni.
Mkuu wa chuo hicho, Profesa Joe Lugalla amesema chuo hicho ni cha kimataifa na kinawafundisha wanafunzi kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki zikiwamo za Uganda na Kenya .
Kwa mujibu wa Profesa Lugalla ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Elimu Afrika Mashariki ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU -IED,EA), amesema jumla wanafunzi 47 waliohitimu, 25 kati yao ni wa ngazi ya shahada ya uuguzi na ukunga na shahada ya uzamili ya ualimu ni 22.
Mbali na hilo, Profesa Lugalla amesema suala la elimu na afya ni muhimu kwa Taifa linaloendelea ndiyo maana AKU imejikita katika kuiboresha elimu.
"Tunaamini watu wakielimika wana uwezo wa kutambua matatizo yanayowakabili yanayohusiana na maendeleo. Tukiwa watu wenye afya bora ni muhimu kwa sababu wataweza kutoa mchango wa maendeleo kwenye jamii zao," amesema Profesa Lugalla.
Mmoja wa wahitimu wa fani ya ukunga na uuguzi, Sofia Sanga amesema amefurahi kuhitimu ingawa haikuwa kazi rahisi na inahitaji mtu kujitoa kwa moyo wote na anamshukuru Mungu kuhitimu salama.
"Nitaingia kazini na moyo mwingine nikimpa mgonjwa nafasi ya kwanza kabla ya kitu chochote. Vilevile kwa wale wauguzi wasiotaka kufanya kazi vijijini watambue magonjwa yapo mahali popote haijalishi upo mjini au vijijini wasiangalie masilahi bali wafuate itikadi ya kazi ya ambayo inampa nafasi ya kwanza mgonjwa kabla ya kitu kingine," amesema Sanga.
0 Comments