HOJA HII IGUSE SHULE ZOTE ZA SERIKALI NCHINI


       
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi)
   
Kwa ufupi

Matokeo hayo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde yanaonyesha kiwango cha ufaulu kimeongezeka kwa asilimia saba ukilinganisha na ufaulu wa 2016.

 Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Oktoba/Novemba mwaka jana yametangazwa huku shule binafsi zikiendelea kufanya vizuri ikilinganishwa na zile za Serikali. Matokeo hayo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde yanaonyesha kiwango cha ufaulu kimeongezeka kwa asilimia saba ukilinganisha na ufaulu wa 2016.

Katika matokeo hayo, Dk Msonde pia alieleza kuongezeka kwa udanganyifu ambao umewagharimu watahiniwa 265 kwa kufutiwa matokeo. Katika matokeo hayo, shule za Serikali zimeendelea kuwa nje ya kundi la shule 10 bora.

Kibaya zaidi, katika matokeo ya shule ya Serikali ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu ya Viziwi Njombe, watahiniwa wake wote 21 wamepata daraja sifuri. Matokeo hayo yalimlazimu mbunge wa Buyungu, Samson Bilago kuuliza swali jana bungeni akiitaka Serikali kutoa maelezo.

Katika majibu yake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Joseph Kakunda alitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Manispaa ya Njombe, kufanya uchunguzi wa kutafuta chanzo cha wanafunzi hao wote kupata daraja sifuri.

Tunapongeza hatua iliyochukuliwa na Naibu Waziri Kakunda ambaye katika wizara hiyo anashughulikia eneo la elimu, kitendo cha wanafunzi wote kupata daraja sifuri ni aibu hata kwa manispaa yenyewe.

Tunaamini uongozi wa manispaa hiyo utapokea maelekezo hayo na kuyafanya fursa ya kufanya vizuri zaidi kwa shule hiyo na nyingine za Serikali mkoani humo.

Ushauri wetu, maelekezo ya Naibu Waziri Kakunda yaongezwe wigo kwa kuhusisha shule zingine za Serikali nchini ambazo zimekuwa na ufaulu duni. Mfano, katika kundi la shule 10 bora kitaifa, hakuna hata moja ya Serikali na kwa miaka kadhaa sasa, shule binafsi zimekuwa zikitamba kwenye kundi hilo.

Hata kwenye kundi la wanafunzi 10 bora kitaifa, shule za Serikali zimekuwa zikisuasua. Walau katika matokeo ya juzi, shule ya sekondari ya Ilboru imefanikiwa kuingiza wanafunzi watatu kwenye kundi hilo.

Rai yetu kwa Naibu Waziri Kakunda ni kuongeza wigo wa maelekezo yake kwa kuzitaka shule zote za Serikali zilizofanya vizuri zifanye uchunguzi wa sababu za mafanikio hayo na kuyatengenezea mkakati wa kufanya vizuri zaidi katika mitihani ijayo.

Vivyohivyo kwa shule zilizofanya vibaya ni muhimu nazo zikafanya uchunguzi utakaoziwezesha kujua sababu za kufanya vibaya, na changamoto watakazobaini wazigeuze fursa kwa kuzitengenezea mikakati itakayowawezesha kutoka hapo zilipo.

Tunaamini kauli ya Naibu Waziri Kakunda itakuwa chachu kwa shule zote za Serikali nchini kujitathmini na kuangalia njia bora ya kuwa na ufaulu mzuri kwa watahiniwa wao katika mitihani ijayo ya taifa.

Serikali sasa hivi inatoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari ikiwamo kuondolewa kwa michango ya aina yoyote, hivyo ombi letu kwa viongozi wa manispaa na wale wote wanaosimamia elimu, wasiwe chanzo cha kukwamisha lengo zuri la Serikali katika kuimarisha sekta hii adhimu.

Tunawaomba wanaosimamia elimu katika mikoa yote nchini kuziwezesha shule hizi kuwa na ufaulu mzuri, tunaamini jitihada zao ndiyo mafanikio ya elimu bure nchini.     

     
 

0 Comments