HARAMBEE YA KUJENGA SHULE YA SEKONDARI LINDI INATARAJIWA KUKUSANYA BILIONI 1

RAIS mstaafu, Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika harambee ya kukusanya fedha kiasi cha Sh. bilioni moja, kwa ajili ya ukarabati wa Shule ya Sekondari Lindi iliyoungua Julai 2016.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema harambee hiyo itafanyika kesho jijini Dar es Salaam.

Zambi alisema maandalizi yote kwa ajili ya harambee hiyo yamekamilika na inatarajia kuhudhuriwa na wadau wa sekta ya elimu nchini.

Alisema harambee hiyo imepanga kukusanya Sh. bilioni moja ikiwa ni karibu nusu ya mahitaji ya Sh. bilioni mbili zinazotakiwa kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo kongwe.

“Kutokana na fedha tutakazokusanya, tumepanga ujenzi uanze wakati wowote. Zoezi hili litakwenda sambamba na mpango wa mkoa kuboresha mfumo mzima wa masuala ya elimu toka ngazi ya awali,” alisema Zambi.

Mkuu wa mkoa huyo alikiri kuwa mkoa wake ni mmoja kati ya inayofanya vibaya kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa, lakini akasema hatua zimechukuliwa kurekebisha, ikiwamo kupima uwezo wa walimu.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu wa Mkoa huo, Emmy Mchuchuri, alitaja changamoto zinazoukabili mkoa huo katika kutoa elimu kuwa ni miundombinu mibovu, uzembe wa walimu, utoro na kutokuwapo kwa chakula cha mchana shuleni.

Alisema ofisi yake imeanza kutekeleza maazimio ya wadau juu ya namna bora ya kuboresha elimu ndani ya mkoa huo, ikiwamo utoaji wa chakula cha mchana shuleni na mafunzo kwa walimu, ili kujenga uwezo wao wa ufundishaji.Alisema walimu watakaobainika kuwa na viwango vidogo vya ufundishaji watashushwa madaraja yao.

0 Comments