MWANAFUNZI ALIYETOWEKA AJISALIMISHA POLISI - IRINGA


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Juma Bwire akizungumza.

MWENYEKITI wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo amefikishwa makao makuu ya Polisi Mkoa wa Iringa Mjini Iringa kwa mahojiano zaidi wakati jeshi hilo likiendelea na uchunguzi wa taarifa zake za kutekwa na watu wasiojulikana mapema wiki hii.

Mwanafunzi huyo wa mwaka wa tatu wa kitivo cha Siasa na Utawala cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anadaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha Jumanne usiku akiwa jijini Dar es Salaam na akaonekana asubuhi ya Jumatano ya Machi 7 mjini Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa baada ya kwenda kutoa taarifa hiyo Polisi.

Leo majira ya saa 4.45 asubuhi, mwanafunzi huyo alifikishwa makao makuu ya polisi mkoani Iringa akiwa katika gari dogo binafsi aina ya Toyota Porte lenye namba za usajili T 256 DDW akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa polisi watatu akitokea kituo cha polisi cha Mafinga.

Akizungumza na wanahabari kwa sharti la kutoulizwa swali lolote ili kutovuruga uchunguzi wa tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Juma Bwire alisema, mwanafunzi huyo alifika katika kituo kidogo cha Polisi cha Mjini Mafinga jana Jumatano, majira ya saa 1.00 asubuhi na kueleza kwamba alitekwa na watu wasiojulikana.

Alisema Jeshi la Polisi limefungua jalada la uchunguzi na limejipanga kuchukua hatua stahiki ikiwemo ya kuwasaka na kuwafikisha katika vyombo vya dola, watuhumiwa watakaobainika kuhusika na tukio hilo.

Na kama atakuwa ametoa taarifa za uongo kwa nia ovu, Kamanda Bwire alisema mwanafunzi huyo atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Tunaendelea kumuhoji mwanafunzi huyu na kama mnavyomuona mbele yenu hali yake ni nzuri, hana majeraha wala makovu na afya yake ni nzuri,” alisema huku akizuia pia mwanafunzi huyo kuulizwa swali lolote akisema hiyo itasaidia kutovuruga uchunguzi unaoendelea.

Aliwaomba wananchi wenye taarifa zozote zinazohusina na tukio hilo kujitokeza kutoa ushirikiano ili kukamilisha suala hilo kwa wakati.

Taarifa iliyotolewa na TSNP mbele ya baba mdogo wa mwanafunzi huyo na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari jana, ilisema kiongozi huyo wa wanafunzi alionekana mara ya mwisho mnamo Jumanne katika ofisi za shirika hilo eneo la Sinza, Dar es Salaam alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa iliyokuwa imetolewa na shirikisho la vyuo vikuu nchini humo, Tahliso.

Muungano huo ulisema baada ya kuondoka katika ofisi hizo, Nondo alielekea chuoni na kuaga kuwa anaondoka kwenda nyumbani Madale.

“Ghafla katika hali ya kutatanisha, kuanzia saa 6 hadi saa 8 usiku alijitoa kwenye makundi yote ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp jambo lililozua taharuki miongoni mwa watu wengi na kuanza kutaka kujua nini kimemsibu,” muungano huo ulisema kupitia taarifa yao.

“Saa 9.09 usiku alituma ujumbe mfupi kwa Mkurugenzi wa Idara ya Sheria TSNP Paul Kisabo ujumbe uliosomeka 'Am at risk!' [Nimo hatarini].”

Taarifa ya chama hicho cha wanafunzi inasema Nondo amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana

0 Comments