Kwa ufupi
Mtoto huyo wa miaka 10 alitoa taarifa hizo kituo cha polisi, akitaka shamba kutouzwa kwa kuwa familia yao ina maisha duni
Dar es Salaam. Rais wa Mtandao wa Wasanii wa Injili na Maadili ya Utaifa (Tagoane), Dk Godwin Maimu amesema wanamkatia bima ya afya mtoto Anthony Petro (10), aliyemshtaki baba yake asiuze shamba la familia Wilaya ya Ngara Mkoa wa Kagera.
Amesema wamechukua uamuzi huo baada ya kuguswa na maisha ya mtoto huyo na kuamua kumkatia bima ya afya pamoja na wadogo zake wawili.
Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 10 ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Ngundusi, Kata ya Kabanga.
Hivi karibuni mtoto huyo aliiteka mitandao ya kijamii na vyombo vya habari baada ya kusambaa kwa video yake, akielezea namna alivyomshtaki baba yake katika kituo cha polisi Kabanga asiuze shamba na wao kukosa ardhi.
Amesema wanaishi maisha ya dhiki wakimtegemea baba yao anayejishughulisha na kilimo na kuokota chupa za plastiki mitaani ili kupata chakula.
Akizungumza na MCL Digital, leo Machi 29, 2018, Dk Maimu amesema baada ya kusoma habari za mtoto huyo katika gazeti la Mwananchi, waligundua moja ya huduma muhimu anazohitaji ni uhakika wa afya yake.
“Tumeanza mawasiliano na Mfuko wa Bima ya Afya na taratibu zote za msingi zitakapokamilika basi tutakwenda Ngara,” amesema.
“Tumeamua kusema jambo hili wakati tunapoanza taratibu ili kama kuna wengine wanafikiria kuhusu bima zao za afya waangalie kitu kingine cha kuwasaidia na ninashauri watume pesa kupitia akaunti ya Mwananchi inayotangazwa kwenye gazeti.”
Amesema watoto wengi vipaji na uwezo mzuri wamekuwa wakipotelea gizani kwa kukosa watu wa kuwasaidia kutokana na uduni wa maisha ya familia zao.
“Mtoto huyu ni tunu ya Taifa, Mungu ameamua kutuonyesha Watanzania kwa hiyo kila mtu kwa nafasi yake anawajibu wa kutimiza ndoto zake, tulishukuru Gazeti la Mwananchi kwa kusaidia kumfuchua,” amesema.
0 Comments