WALIMU WAONYWA KUWAGEUZA WANAFUNZI VITEGA UCHUMI


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William ole Nasha

SERIKALI imesema itawachukulia hatua kali za kinadhamu walimu wakuu na wakuu wa shule za sekondari watakaobainika kuwatumia wanafunzi kama kitega uchumi.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William ole Nasha, alisema hayo alipozungumza na wakuu wa shule za sekondari mkoani Tabora. Alisema serikali imekusudia kutoa elimu bure kwa watoto wote kuanzia shule za awali hadi kidato cha nne hivyo, ni vema wanaowatumia wanafunzi kwenye shughuli za kuzalisha kipato, waache haraka. “Natoa onyo kwa wakuu wa shule wanaowatumia wanafunzi kwenye shughuli za kujiingizia kipato,” alisema.

Alisema kwamba serikali imekusudia kuweka mazingira bora na mazuri kwa kujenga majengo na ofisi kwa shule mbalimbali nchini ili shule ziwe na mazingira mazuri ya kutolea na kupokea elimu. Ofisa Elimu mkoa wa Tabora Suzana Nusu alimweleza Naibu Waziri kwamba katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2017, mkoa wa Tabora ulishika nafasi ya tatu kitaifa kati ya mikoa 31.

0 Comments