MGONGO GOLD MINE YAGANGA DARASA SHULE YA MSINGI KIBULULU - IRAMBA





WANAFUNZI 99 wa darasa la awali katika shule ya msingi Kibululu,kata ya Mgongo,tarafa ya Shelui,wilayani Iramba,Mkoani Singida wanasoma wakiwa wamekaa chini ya miti huku wakitumia magoti ya miguu yao kama meza wakati wakiandika kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa pamoja na madawati unaoikabili shule hiyo.


Kaimu Ofisa elimu Kata ya Mgongo,Lazaro Isaya Sakata alithibitisha kuwepo kwa upungufu huo wa vyumba vya madarasa pamoja na madawati kwenye hafla fupi ya kupokea tani tano za mifuko ya saruji zilizotolewa na Kampuni ya kuchimba madini ya Mgongo Gold Mine kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo.


Alifafanua Ofisa huyo wa elimu kuwa wanafunzi wa awali katika shule ya msingi Kibululu wanasoma wakiwa wamekaa chini ya miti kwa sababu hakuna chumba cha darasa kinachoweza kuwamudu kuingia wote 99 na kuweza kumsikiliza mwalimu wao kikamilifu.


Kwa mujibu wa Sakata wanafunzi hao 99 wanatakiwa kuwa na vyumba vinne vya madarasa kutokana na kwamba uwiano wa mkondo mmoja ni wanafunzi 25,kitu ambacho kimekuwa kigumu na kulazimika kuwakusanya chini ya miti na kuendelea na masomo.


“Sasa namna ya kumudu kwamba niangalie kila mmoja anaumba vipi ile herufi au kile ninachokifundisha,inakuwa ni kazi kidogo mara kuna mvua mnatoka mnakimbia,mara jua kali inabidi msogee mahali Fulani na mara kuna upepo kwa wakati wote wanakuwa ni vurugu halafu mkiwa nje watoto hawajifunzi vizuri”alisisitiza Sakata.


Akikabidhi msaada huo wa tani tano za saruji,Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mgongo Gold Mine,Herieth Michael Sagati alitumia fursa hiyo kuyashawishi Makampuni yanayochimba madini katika Kijiji cha Kibululu kujitokeza na kuhakikisha wanawekeza kwenye sekta ya elimu.


Kwa mujibu Mkurugenzi huyo endapo wawekezaji hao watajikita zaidi katika sekta ya elimu watakuwa wamewapatia watoto urithi wa maisha kuliko hata urithi wa fedha,majengo na hata mali nyinginezo walizonazo na kwamba uwekezaji huo utakuwa wa kudumu na hautasahaulika hata mbinguni.


Naye mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya MGM,Gabrieli Issah alibainisha kuwa msaada huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1.8 ni utekelezaji wa ahadi waliyotoa ambayo pia ni sera ya nchi kwamba kila mwananchi anayejihusisha na uchimba,lazima maeneo yanayozunguka machimbo hayo yaweze kufaidika na uchimbaji huo.

Akipokea msaada huo,Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kibululu,Mwanjaa Danieli Mkoma aliweka wazi kwamba katika mitihani ya taifa ya kumaliza elimu ya msingi mwaka jana,asilimia 26 ya wanafunzi 78 waliofanya mitihani ndiyo waliofanya vizuri huku asilimia 74 walifanya vibaya.

Kata ya Mgongo ina shule za msingi tano zikiwepo nne shule nne za msingi na moja ya sekondari na kwamba hakuna shule ya msingi inayojitosheleza kwa vyumba vya madarasa pamoja na madawati wakati kwa shule ya msingi Kibululu ina upungufu wa nyumba za walimu 8 vyumba vya madarasa vinane.

Ni baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Kibululu,kata ya Mgongo,wilayani Iramba wakionekana wakipanda juu ya gari dogo lililoleta saruji kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa ambayo yameonekana kuwa ni changamoto kwa wanafunzi kusomea chini ili waweze kushusha mzigo huo.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mgongo Gold Mine,Herieth Sagati akiwa na wanafunzi wa shule ya msingi Kibululu,kata ya Mgongo katika picha ya pamoja mara baada ya gari lililobeba saruji kuwasili shuleni hapo

0 Comments