SERIKALI YATOA UFAFANUZI KUHUSU ADA YA MITIHANI KWA SHULE BINAFSI

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema wanafunzi wanaosoma katika shule binafasi wataendelea kutozwa ada ya mitihani ya taifa kwa kuwa programu ya elimu bila malipo haizihusu shule hizo hivyo wazazi na walezi ni jukumu lao kugharamia huduma hizo.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 15, 2018 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 29 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu la Mbunge Viti Maalum Ester Mahawe aliyetaka kujua ni lini serikali itafuta ada ya mitihani ya Taifa kwa shule za msingi na sekondari kwa wanafunzi wanaosoma katika shule binafsi ?.

"Serikali inatambua umuhimu wa sekta binafsi katika utoaji elimu nchini. Ili kuhakikisha mazingira rafiki katika utoaji wa elimu serikali imekuwa ikifanya majadiliano na sekta binafsi kwa lengo la kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabiri. 

"Katika utekelezaji wa mpango wa elimu bila ya malipo, serikali ilifuta ada na michango ya lazima katika shule za umma ngazi ya elimu msingi hadi kidato cha nne", amesema Olenasha

Pamoja na hayo, Naibu Waziri Olenasha ameendelea kwa kusema "ada na michango hiyo iliyokuwa inalipwa na wazazi au walezi kwasasa inagharamiwa na serikali, mpango huu haujazihusisha shule binafsi pamoja na umma ngazi ya kidato cha tano na sita. Hivyo shule hizo zitaendelea na utaratibu wa wazazi au walezi kulipa ada za mitihani ya Taifa".

Kwa upande mwingine, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu nchini kadri uwezo wa kifedha utakaporuhusu kufanya hivyo.

0 Comments