WANAFUNZI WA DIPLOMA KUPEWA MIKOPO - HESLB





BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imepanua wigo wa utoaji wa mikopo hiyo, kwa kuanza kuitoa kwa wanafunzi wa diploma, hasa kwenye fani zenye uhitaji zaidi.

Bodi hiyo kwa mwaka huu imeongezewa fedha zaidi za mikopo, kwa kupewa Sh bilioni 427 na hivyo kuongeza idadi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza kupatiwa mikopo hiyo kutoka 33,000 kwa mwaka jana hadi wanafunzi 40,000 mwaka huu. Hayo yalibainishwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Abdul-Razak Badru wakati akizungumzia mwongozo mpya wa uombaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, ambapo kwa mwaka huu bodi hiyo imetoa muda wa mwezi mmoja na wiki mbili kuomba mikopo hiyo.

Alisema kwa miaka iliyopita, Bodi ilikuwa ikitoa mikopo kwa waombaji wa masomo ya ngazi ya diploma kwenye fani ya Ualimu peke yake, lakini kwa mwaka huu imeongeza wigo zaidi kwa kuanza kupokea pia maombi kwenye fani za aina zote za Uhandisi kuanzia Sayansi za Kilimo, Wanyama, Gesi na Sayansi ya Afya ya Binadamu. Badru alisema, uamuzi huo unatokana na nia ya serikali ya kuwa na Tanzania ya Viwanda, ambapo fani hizo ni muhimu katika kufanikisha mkakati huo kwa kuwa wafanyakazi wenye Stashahada ndio watendaji wakubwa zaidi.

Alisema kwa waombaji wa ngazi ya Shahada, Bodi itatoa kipaumbele kwa waombaji wa fani kama hizo za Uhandisi, ambazo kwa sasa zina uhitaji zaidi huku akizitaka familia zenye uwezo wa kuwasomesha watoto wao kutoomba mikopo hiyo ili waliotokea familia masikini wanufaike kwa wingi zaidi. Alisema, kwa kushirikiana na Wakala Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), wanafunzi yatima watakaothibitishwa na wakala huo watapewa mikopo huku akiwataka waombaji wenye ulemavu kuwa na barua ya uthibitisho kutoka kwa Mganga wa Mkoa au Wilaya, huku na kwa waombaji waliofadhiliwa masomo ya Stashahada au sekondari, wanatakiwa kuwa na barua za uthibitisho kutokea taasisi zilizowasomesha.

Akizungumzia zaidi kuhusu mfumo wa sasa wa kufanyia maombi hayo, alisema mwombaji atajijua kama amefanikiwa kutuma maombi kwa usahihi iwapo atajibu maswali 21 atakayoulizwa kwenye akaunti yake atakayofungua kwenye tovuti ya Bodi. Alisema, ili kutoka kwenye hatua ya kwanza ya kuomba kwenda nyingine, ni lazima hatua ya awali awe ameijibu vema na ndipo itafunguka hatua nyingine na mwisho wa siku kujibiwa kuwa amefanikiwa kutuma maombi. Meneja wa Usajili kutokea Rita, Patricia Mkuya, aliwataka wanafunzi yatima wenye nia ya kuomba mkopo huo wawasilishe nakala za vifo vya wazazi au mzazi mmojawapo kwenye ofisi za Rita kwenye mkoa au wilaya walizopo wahakikiwe

0 Comments