ZAWADI, LIFTI VINAWAPONZA WANAFUNZI WAKIKE


KUMEKUWA na madai ya muda mrefu kwamba madereva na makondakta wa daladala, madereva wa bodaboda na pikipiki kikwazo kikubwa kwa watoto wa kike walioko shuleni.
Inadaiwa kupitia ‘lifti’ wanazopewa na watendaji hao wa vyombo vya usafiri na wakati mwingine ulaghai wa fedha na zawadi, huwafanya watoto hao kunasa katika mitego ya kimapenzi na kujikuta wakishindwa kumaliza masomo kwa kupata ujauzito au kuolewa katika umri mdogo.
Ili kuwanusuru watoto wa shule na kadhia hiyo, Shirika la Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (Wajiki), limeanzisha klabu shuleni kusaidia kutatua tatizo hilo.
Katika klabu hizo, watoto huweka wazi changamoto wanazokutana nazo kwenye vyombo vya usafiri na kujadiliana athari zake na namna ya kupambana nazo. Mkurugenzi wa Wajiki, Janeth Mawinza anasema shirika lao linafadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake Tanzania (WFT).
Mawinza anasema miongoni mwa mambo ambayo watoto wamekuwa wakieleza kukumbana nayo, ni kurubuniwa na baadhi ya madereva pamoja na makondakta.
Anasema pia shirika limekuwa likikutana na wanawake waliotelekezwa na waume zao au wale waliozaa nao.
Katika mazungumzo wengi wao hulalamikia makondakta na madereva wa daladala kuwa wametelekeza watoto waliozaa nao.
Kutokana na matukio hayo, shirika hilo limekuwa likiwajengea uelewa madereva na makondakta wafahamu athari za ngono na kutambua wajibu wao wa kuwa walezi pale wanaposababisha ujauzito.
Hivyo, katika kuanzisha klabu hizo shuleni wamezungumza na shule mbili; Shule ya msingi ya Mchangani na sekondari ya Makumbusho, zilizopo jijini Dar es Salaam. Lakini lengo lao hasa anasema ni kuanzisha klabu hizo kwa shule zote za kata ya Makumbusho, Mwananyamala na Kawe.
Salum Hamza ni dereva wa daladala kutoka Umoja wa Madereva Tegeta na Bunju (Uwamatebu) anayezungumzia madai hayo.
Anasema matukio ya madereva kufanya ngono na watoto wa shule kwa sasa yamepungua kutokana na kuwepo kwa sheria kali za serikali pamoja na majukumu makubwa ya familia waliyo nayo madereva.
Anakiri kuwa kipato ni miongoni mwa vichocheo vya baadhi ya kufanya ushawishi kwa watoto wa kike.
Hata hivyo anasema hivi sasa kipato kimepungua kutokana na wingi wa daladala uliopo. Kwa mujibu wa Hamza, hivi sasa kipato cha dereva hakimpi ushawishi wa kufanya vitu kama hivyo.
Miongoni mwa mambo yanayochangia kushuka kwa kipato ni kupanda kwa mafuta tofauti na zamani.
“Hivyo dereva anapambana kutafuta hela ya mafuta kwanza,” anasema na kuongeza kuwa katika takribani miaka mitano iliyopita, magari hayakuwa mengi hivyo kwa mtu aliyekuwa akifanya shughuli ya usafirishaji alikuwa na uhakika wa kipato kikubwa.
“Zamani kulikuwa na njia ya Bunju –Mwenge pekee lakini sasa hivi kuna njia sita katika barabara hiyo ya Bagamoyo, hivyo madereva wote tunagombea abiria hao hao,” anasema.
Dereva wa bodaboda anayefanya shughuli zake Mwananyamala A, jijini Dar es Salaam, Suleiman Lasway anakiri kuwepo baadhi ya wanaorubuni wanafunzi wa kike.
Anasema wenye tabia hiyo, hutumia fursa ya kumpeleka mwanafunzi bure bila kulipa nauli, hali inayoleta mazoea na mwishowe, huibuka tamaa ya ngono. Lakini Lasway analaumu pia baadhi ya wanafunzi akisema, wengi wanakuwa na tamaa ya fedha.
“…Kwa sababu ya kufanya mashindano na wenzao katika kula chipsi, ama vitu vya anasa kama simu na vipodozi ambavyo siyo rahisi mzazi kuvibaini kwa haraka,” anasema.
Dereva huyo wa bodaboda anakubaliana na mkakati wa kutoa mafunzo kwa wanafunzi ili wapate uelewa waachane na tamaa. Anapongeza kuanzishwa kwa klabu hizo shuleni kwamba zitakuwa ni mkombozi kwa wanafunzi hao wa kike.
“Kuna mwenzetu mmoja hapa kijiweni alimlaghai mwanafunzi wa darasa la tano, lakini alipoanza kufuatiliwa akakimbia na kuacha kijiwe. Lakini hili pia linachangiwa na wanafunzi wenyewe wa kike kwa kuwa na tamaa ya vitu ilhali uwezo hawana,” anasema.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Margaret Mussai anasema hakuna atakayeachwa nyuma katika mapambano ya kumkomboa mtoto wa kike.
Mussai anasema, kubadili mawazo ya mtu ni kazi kubwa, hivyo jitihada zinazofanywa na shirika hilo siyo za kupata majibu kwa mara moja. Anashauri jamii kusaidiana na wadau wa kumkomboa mtoto wa kike ili kuepusha athari mbalimbali zinazoweza kutokea.
“Maendeleo ya jamii ni kazi yetu. Wadau tushikamane na Wajiki,” anasema na kuongeza haipendezi kusikia mtoto amebakwa ndio tunaanza kukimbizana.
Anashauri wazazi wawe na muda na watoto wao. “Siku hizi wazazi wengi wanatoka asubuhi; hawana muda na watoto na kurudi usiku. Watoto ni wetu lazima tuwalee,” anasema.
Anasema mwaka 2011, watoto walifanyiwa utafiti na kubainika kuwa wanafanyiwa vitendo vya ukatili shuleni mara 40 na nyumbani mara 20. Anasema rushwa ya ngono ni miongoni mwa rushwa nyingi zinazowafanya watoto wasisonge mbele.
Anasisitiza umuhimu wa kupita shule hadi shule kuwezesha wasichana kujitambua.

0 Comments