Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Stella Ikupa.
Kwa ufupi
Ikupa amesema asilimia 98 ya Watanzania hawajui lugha ya alama na asilimia mbili iliyopo hawapewi nafasi.
Dodoma. Serikali imetaja uhaba wa wakalimani wa lugha ya alama kama chanzo cha kuwanyima haki wenye uziwi na hata katika vyombo vya ulinzi.
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 2 na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Stella Ikupa wakati akifungua mkutano wa kitaifa wa ushawishi na utetezi wa lugha ya alama ulioratibiwa na Chama cha Walimu wenye Uziwi Tanzania.
Mkutano huo ulifadhiliwa na Shirika la The Foundation for Civil Society (FCS), ukiwa na lengo la kutafuta lugha ya pamoja katika vyombo muhimu kama magereza, polisi na mahakama.
Ikupa amesema asilimia 98 ya Watanzania hawajui lugha ya alama na asilimia mbili iliyopo hawapewi nafasi pana, kusikilizwa na kutoa mchango wao kwa weye mahitaji.
Amesema jambo hilo limewafanya wenye ulemavu kutengwa na ndicho chanzo cha wengine kushindwa kutafuta haki zao kwa kutoripoti katika vyombo vya ulinzi na usalama matukio mbalimbali wanayofanyiwa na jamii.
“Wakalimani wa lugha ni wachache, lakini asilimia 98 ya Watanzania hawajui kutumia lugha za alama na hivyo kujikuta ndugu na jamaa zao kutengwa na kukoseshwa haki zao,” amesema Ikupa.
Naibu waziri amewataka viongozi wa magereza na polisi kuweka wakalimani maalumu sehemu zao za kazi ambao wataangalia namna ya kuwapa haki watu wenye ulemavu mara wanapofika kutafuta huduma.
Meneja mipango wa Shirika la The Foundation for Civil Society Francis Uhadi, amesema waliamua kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia mafunzo hayo ambayo yatawaweka pamoja Watanzania ili kupunguza tatizo hilo ambalo limesababisha kundi hilo kuwa nyuma zaidi.
Uhadi amesema kuna changamoto ya kukamatwa na kukosa haki zao kutokana na kushindwa kuwasiliana na watoa maamuzi.
Mwakilishi wa shirika lisilo la kiserikali la Institutions For Inclusive Development (I4ID), Maisoli Chacha amesema wameungana na walimu wenye uziwi ili kutafuta dawa ya kumaliza matatizo ya lugha za alama.
Chacha amesema matokeo mabaya ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Njombe ambapo walipata alama sifuri ndiyo hasa yaliyowaamsha wadau na hawatarajii kupata matokeo kama hayo tena.
Ad
0 Comments