Warioba alisema hayo jana wakati akizungumza na
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kwenye Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar
es Salaam.
“Kutunga Katiba ya Tanganyika siyo kazi ngumu,
ukisoma rasimu hii sura ya kwanza mpaka ya tano, sioni kama Katiba ya
Tanganyika itakuwa tofauti na maoni yaliyomo katika sura hizo,” alisema
na kuongeza:
“Misingi iliyopo katika utangulizi wa rasimu hii
imetokana na maoni ya wananchi hao. Wakati wa kukusanya maoni, Zanzibar
walijikita zaidi kwenye Muungano, maoni mengine kwa kiwango kikubwa
yametoka kwa Watanzania Bara na katika kuandika Katiba ya Tanganyika
sioni kama watabadilisha chochote kuhusu misingi hii ambayo ni; tunu za
taifa, maadili, malengo na haki za binadamu.”
Alisema kuhusu kubadilishwa kwa mihimili ya
Serikali na vyombo vingine vya kitaifa, kikubwa kinachoweza kuguswa ni
muundo wa Bunge la Tanganyika, Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Baraza
la Mawaziri.
“Kuhusu taratibu za kufanya kazi; iwe ni madaraka
ya Rais, utaratibu wa kufanya kazi katika Bunge, Mahakama na Serikali
sioni kama litakuja suala jipya kwa sababu mambo hayo yameshatolewa
maoni. “Kilichobaki ni madaraka kwa umma tu, kwa maana ya Local
Government (Serikali za Mitaa). Hata hili la madaraka kwa umma
watakaolishughulikia watumie taarifa za wananchi waliotoa maoni yao
kuhusu Katiba Mpya. Wananchi walitoa maoni kuhusu jambo hili ambayo yapo
wazi kabisa.”
Uchaguzi Mkuu 2015
Kuhusu uwezekano wa Katiba Mpya kutumika katika
Uchaguzi Mkuu 2015, Jaji Warioba alisema Tume hiyo ilipewa muda mfupi wa
kuandaa Rasimu ya Katiba kwa sababu ilielezwa kuwa uchaguzi wa mwaka
2015, utafanyika kwa kutumia Katiba Mpya.
“Katiba hii ilitakiwa iwe imekamilika Aprili mwaka
huu, maana yake tungekuwa na mwaka mmoja na nusu wa kufanya mambo
mengine ya kuwezesha itumike kwenye uchaguzi wa mwaka 2015,” alisema.
Alisema ndiyo maana katika rasimu hiyo, Tume
imeweka masharti ya mpito ya miaka minne, kuanzia siku inapopatikana
Katiba Mpya hadi Desemba 28, 2018.
Alisema rasimu hiyo imefafanua Baraza la Mawaziri
na Bunge vitakuwaje… “Sasa hivi tuna Serikali na Bunge. Katiba Mpya
itapatikana mwaka huu, lakini Bunge letu litaendelea kuwapo kwa msingi
wa Katiba ya sasa mpaka ufike wakati wa uchaguzi, hiyo inafanyika kwa
ajili ya kulinda uongozi wa Bunge na Serikali.”
Alisema ili kuwepo na Uchaguzi Mkuu kwa Katiba
Mpya ni lazima itungwe Katiba ya Tanganyika, kwamba wamependekeza miaka
minne ya mpito ili kutoa nafasi ya kubadilishwa kwa mambo kadhaa, ikiwa
ni pamoja na kuundwa upya Tume ya Uchaguzi itakayoendesha uchaguzi kwa
msingi wa Katiba Mpya.
“Siyo lazima kila kitu kikamilike baada ya miaka minne, kuna
mambo yanaweza kubadilishwa kwa miezi sita au mwaka mmoja. Kila
tulipobadili Katiba tulifanya jambo hili.
“Mfano ni mwaka 1984 tulipofanya mabadiliko
makubwa ya Katiba ambayo ilileta ukomo wa Rais, haki za binadamu, waziri
mkuu na mambo mengine makubwa. Kipindi hicho ilitungwa sheria mpya ya
uchaguzi ambayo inatumika hadi sasa.”
Gharama Serikali tatu
Kuhusu hoja kwamba muundo wa Serikali tatu ni
gharama, Jaji Warioba alisema hautakuwa na gharama kubwa kama
inavyotafsiriwa na watu wengi.
Alisema kwa kulitambua hilo, ndiyo maana Tume
ilipunguza ukubwa wa Serikali, ikiwa ni pamoja na kupendekeza idadi ya
wabunge 75 na mawaziri wasiozidi 15.
“Hata uwepo wa Serikali mbili bado hautaweza
kupunguza gharama. Katika hili ni muhimu kukubaliana na mawazo ya
wananchi juu ya muundo wa Serikali tatu ambazo zimepunguza gharama.
Tumependekeza Serikali ya Muungano kuwa na chanzo chake cha mapato
ambayo ni ushuru wa bidhaa, mapato yasiyo ya kodi, michango kutoka nchi
wahisani, mikopo na mapato mengine.”
“Wapo watu wanataka kugawa mikoa, wapo
wanaopendekeza Jiji la Mbeya ligawanywe, wapo wanaotaka Songea
igawanywe, hizi zote ni gharama… Sasa iweje kugawa mikoa isiwe gharama,
Serikali tatu iwe na gharama? Hata kijiji ninachotoka zamani kilikuwa
kimoja, sasa vimegawanywa vipo vitatu!”
Alisema Tanganyika ilipopata uhuru kulikuwa na
majimbo manane tu, lakini sasa ipo mikoa 25 na wilaya, tarafa na vijiji
zimegawanywa.
Alisema gharama za Serikali ya Muungano zitakuwa
katika Wizara ya Ulinzi na Usalama pamoja na Mambo ya Nje, taasisi
ambazo tayari zipo, “Inashangaza kuona watu wakisema kuwa Tume
kupendekeza Serikali tatu ni kwenda kinyume na mawazo ya Mwalimu Julius
Nyerere.”
Kumsaliti Nyerere
Alisema hata Mwalimu Nyerere hakuwa na mawazo
mgando. Alikuwa anatambua mabadiliko na mara kadhaa alibadilika
kulingana na mahitaji ya wananchi na wakati.
Alitoa mfano akisema Mwalimu Nyerere alikuwa
muumini wa mfumo wa chama kimoja, lakini mwaka 1992 baada ya Ripoti ya
Jaji Francis Nyalali, alibadili mawazo na kuukubali mfumo huo licha ya
asilimia 80 ya Watanzania kuupinga.
Alisema: “Maoni ya msingi yaliyomo katika rasimu hii yametokana
na maoni ya wananchi, lakini vyombo vya habari vimejikita kuzungumzia
mambo yanayohusu uongozi, hasa mambo ya kisiasa,” alisema Warioba huku
akisisitiza kuwa Katiba hiyo siyo mali ya Tume wala kundi fulani katika
jamii.
Alisema wananchi wamezungumzia matatizo ya kilimo,
usafiri, afya, hifadhi ya jamii, maadili katika taifa na haki za
binadamu… “Mambo haya katika kutoa habari hayakupewa kipaumbele, lakini
mambo kuhusu kugombea urais, ubunge yalipewa kipaumbele kikubwa.”
Ukomo na uraia
Alisema tume hiyo inafanya kazi yake kwa kufuata
sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba itamaliza muda wake
itakapowasilisha rasimu hiyo katika Bunge Maalumu la Katiba.
Kuhusu uraia wa nchi mbili alisema:
“Tulipopendekeza suala hili tulikuwa na maana kuwa isiwe lazima
Mtanzania akipata uraia wa nchi nyingine awe amepoteza hadhi yake. Ndiyo
maana tukasema katika rasimu kuwa atakuwa na hadhi maalumu.”
Alisema nchi nyingi duniani hutoa uraia kwa watu
kutoka mataifa mbalimbali lakini hawawezi kugombea urais, kuingia katika
jeshi la nchi husika, kwamba sheria lazima ifafanue juu ya Mtanzania
kutopoteza haki zake za msingi.
0 Comments