WABUNGE wa kuchaguliwa ambao pia ni wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba watapimwa na watanzania kama kweli ni wazalendo kwa nchi yao au
ni wazalendo kwa vyama vyao.
Watapimwa jinsi watakavyokuwa wanachangia ibara mbalimbali za rasimu,
rasimu ambayo inakwenda kuwa katiba ya nchi (sheria mama).
Watanzania wa maeneo wanapotoka wabunge watapimwa Je, anafaa kurudi bungeni 2015?
Kama kweli wabunge wa kuchaguliwa wanaupenda ubunge wao wanatakiwa
wachangie michango yao kama watanzania, sio kama wabunge wa kutoka
chama fulani.
Wabunge mnatakiwa kuingia kwenye Bunge maalumu la katiba mkijua
mnawakilisha watanzania million 43, sio kuwakilisha vyama vyenu vya
siasa, makundi yenu, taasisi zenu, NGO’s zenu, makundi maalumu yenye
malengo yanayofanana au wachawi wenzenu mliwawakilisha.
Kusema ukweli mkiingia na mawazo ya kuwawakilisha makundi
niliyoyataja hapo juu makundi ambayo wamewaingiza hapo hamtarudi
mjengoni tena 2015.
Kumbukeni Watanzania wa 2005 sio hawa wa leo 2015, kwa hiyo kuweni
makini na michango yenu mnapojadili rasimu, rasimu ambayo imetokana na
watanzania na ikumbukwe pia rasimu hii haikutokana na ninyi wabunge wa
Bunge maalumu la katiba.
Mkumbuke pia baadhi yenu wabunge mlichaguliwa kwa madhumuni ya
kutunga sheria na kuisimamia serikali na mmeingizwa katika Bunge hili
na sheria siyo na Watanznaia.
Nikiwa na maana mmebadilisha masharti ya kombati, mashati ya kijani
na bluu na mkavaa nguo za jadi lakini bado ninyi ni wale wale wenye
asili ya kubishana hata kwa jambo dogo sana.
Kubadilisha mashati ya vyama vyenu hakubadishi mawazo yenu mnabaki
wale wale. Sasa msipoacha tabia ya kubishana/kuvutana hata kwa jambo
la ukweli.
Mfano: 1 + 1 = 2 lakini mwingine anaweza akatokea akasema 1 + 1 = 11
halafu mkaanza kubishana na baadaye mbishano/mvutano kuamuliwa kwa 2/3.
Ikitokea 2/3 wamekubaliana 1 + 1 = 11 maana yake 11 itakuwa jibu sahihi, sijui kama watanzania tutawaelewa.
Nawasihi wajumbe wa Bunge maalumu la katiba kuacha kubishana na
kuvutana kwa mambo ambayo yako wazi hasa yale ambayo yana manufaa kwa
watanzania kwani mnawakilisha watu wengine ambao hawana vyama kabisa.
Nawasihi kwa namna ya pekee wajumbe wa Chama tawata (CCM) kwani ninyi ndio mko wengi.
Mkumbuke pia ninyi ni wajumbe wa Bunge la “kihistoria” kwa kuwa
Tanzania hatujawahi kuwa na bunge kama hili tangu tupate uhuru 1961,
kwa hiyo mnayo heshima ya pekee, kwani hili ni bunge la kwanza la
kupitisha rasimu ya watanzania kuwa katiba yao; Mnaombwa kulinda
heshima hiyo ya kipekee.
Aidha napendekeza ili kulinda heshima ya bunge hili, yale mambo
ambayo yanaonekana yana mabishano/mvutano wa hoja kwa mfano aina ya
muungano wanaotaka watanzania na maadili ya viongozi wa umma na yale
yote yatakayoonekana ya mawazo tofauti yasiamuliwe na 2/3 ya wajumbe,
badala yake liundwe jopo la majaji 11 toka nje ya bunge hilo ambalo
litakuwa na kazi ya kupima uzito wa hoja ya mzungumzaji na kutoa alama.
Na mwisho wa mabishano/mvutano majaji watatoa uamuzi wa upande upi
imeonekana una hoja nzito na kwa manufaa ya watanzania wote na uamuzi
huo usionekane kuwa upande umeshindwa, ila hoja yao imekuwa nyepesi na
haina maslahi si tu kwa yule aliyekuwa anatetea jambo au alikuwa
anapinga jambo hilo bali ni watanzania wote.
Kuamua kwa kutumia 2/3 itakuwa ni sawa na mfano wa wanafunzi wawili
wanabishana/wanavutana moja anasema 1 + 1 = 2 na mwingine hesabu hiyo
hiyo ya 1 + 1 = 11 halafu ubishani/mvutano huo uamuliwe kwa kura 2/3 ya
wanafunzi darasani, na aliyesema 1 + 1 = 11 akashinda Je, litakuwa ni
jibu sahihi? Kwa kuwa 2/3 ya wanafunzi wameamua jibu ni 11?
Nia njema ya Rais Kikwete kuwatengenezea watanzania katiba yao
inaweza kugeuka majanga kama wajumbe wa bunge hili la katiba watakuwa
mnabishana na ukweli.
Na kusababisha Rais Kikwete badala ya kuingia katika historia ya
kuwaletea watanzania katiba yao, akaingia kwenye historia nyingine
kabisa ambayo hata mimi siombei kabisa.
Na wataomwingiza katika hoja kati ya historia hizo ni ninyi wabunge wa bunge maalumu la katiba.
Likiundwa jopo la majaji 11 kuamua mambo yenye mvutano badala ya 2/3
litamwingiza Rais Kikwete katika historia nzuri ya kuwapatia watanzania
katiba waitakayo na kusababisha pia wapate Tanzania waitakayo.
Ila mambo yakiamuliwa kwa kura 2/3 utashangaa 1 + 1 = 11 badala ya 1
+ 1 = 2, na kuharibu mchakato mzima wa kumwingiza Rais Kikwete katika
historia na “sisemi ibara zote ziamuliwe jopo la majaji hapana” ninasema
“ibara ambazo zitakuwa na mvutano mkali hasa suala la aina ya muungano
na maadili ya viongozi, “ndiyo maamuzi yake yaamuliwe na jopo la
majaji baada ya kupima uzito wa hoja za pande zinazovutana au kubishana
badala ya kutumia 2/3 ya wajumbe wa bara na Zanzibar.
Pendekezo la kutumia majaji badala ya 2/3 ni kuepuka ushabiki wa
vyama kwa wajumbe kupiga kura kwa upande wa mjumbe wake badala ya
kupigia kura uzito wa hoja kwa manufaa ya watanzania milioni 47.
Jopo la majaji nililopendekeza litoke nje na wajumbe hao lijumuishe
wanasheria, watu wa haki za binadamu, viongozi wa dini na watu
wanaoaminiwa na umma.
Nawatakia kila la heri “Bunge maalumu la Katiba”
0 Comments