Moja ya michoro ya nyumba ilijazwa kwenye Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne mwaka jana wakati wa kutangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana.
Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), limetangaza
Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa kidato cha nne wa 2013, huku ufaulu
ukiongezeka kwa asilimia 15.17.
Matokeo hayo ni ya kwanza tangu kuanza kutumika
kwa mfumo mpya wa upangaji ambao ulipanua wigo wa alama na madaraja,
hivyo kutoa nafasi kubwa zaidi kwa watahiniwa kufaulu.
Licha ya kuanza kutumika kwa mfumo huo, idadi ya
waliofeli imeendelea kuwa kubwa kwani watahiniwa 151,187 sawa na
asilimia 42.91 wamepata sifuri. Kati ya hao, wavulana ni 78,950 sawa na
asilimia 41.54 na wasichana ni 72,237 sawa na asilimia 44.51.
Kadhalika matokeo hayo yameendelea kushuhudia
baadhi ya watahiniwa wakiandika matusi kwenye karatasi zao za majibu,
huku wengine wakichora vitu vya ajabu kwenye mitihani hiyo, huku wengine
wakishindwa kuandika chochote kwenye karatasi hizo.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam,
Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema waliofaulu
mtihani huo ni 235,227 sawa na asilimia 58.25 ya 404,083 ya waliofanya
mtihani huo, ikilinganishwa na 185,940 sawa na asilimia 43.08,
waliofaulu 2012.
Dk Msonde alisema wasichana waliofaulu ni 90,064 sawa na asilimia 55.49 na wavulana ni 111,088 sawa na asilimia 58.45.
Alisema watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani
huo walikuwa ni 427,679 wasichana wakiwa ni 199,123 sawa na asilimia
46.56 na wavulana walikuwa ni 228,556 sawa na asilimia 53.44. Kati yao
watahiniwa wa shule ni 367,163 na watahiniwa wa kujitegemea ni 60,516.
Dk Msonde alisema watahiniwa 23,596 ambao ni sawa na asilimia 5.52 ya waliojiandikisha, hawakufanya mtihani huo.
Dk Msonde alisema matokeo hayo yalipangwa kwa
kutumia alama zilizotangazwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome mwaka jana.
Alama hizo ni A: 75-100, B+:60-74, B:50-59,
C:40-49, D:30-39, E:20-29 na F:0-19. Kabla ya mabadiliko hayo, alama
zilizokuwa zikitumiwa kupanga matokeo ya kidato cha nne ni A:80-100,
B:65-79, C:50-64, D:35-49 na F: 0-34.
Alisema pia alama za maendeleo ya wanafunzi zilizotumika ni 30 huku mtihani wa mwisho ukichangia alama 70.
Kuhusu waliochora na kuandika matusi, Dk Msonde
alisema: “Wengine wamechora nyumba, wengine picha za freemason na
michoro mingine ambayo haiendani na somo husika.”
Hata hivyo, alisema tabia ya kuchora michoro hiyo imepungua ikilinganishwa na 2012.
Ubora wa Ufaulu
Dk Msonde alisema watahiniwa waliofaulu kwa daraja
la kwanza mpaka la tatu ni 74,324 sawa na asilimia 21.09 wakiwamo
wasichana 27,223 sawa na asilimia 16.77 na wavulana 47,101.
Alisema waliopata daraja la kwanza ni 7,579 sawa
na asilimia 2.15 wavulana 5,030 sawa na asilimia 2.65 na wasichana
wakiwa 2,549 sawa na asilimia 1.57, wakati waliopata daraja la pili ni
21,728 sawa na asilimia 6.17, wakiwamo wavulana 14,167, asilimia 7.45 na
wasichana 7,561 ambao ni asilimia 4.66.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa waliopata daraja la
tatu ni 45,017 sawa na asilimia 12.78; wavulana 27,904 sawa na asilimia
14.68 na wasichana 17,113 sawa na asilimia 10.54.
Watahiniwa waliopata daraja la nne ni 126,828 sawa
na asilimia 36 na wavulana wakiwa ni 63,987 na wasichana 62,841 sawa na
asilimia 38.72.
Ubora wa ufaulu kwa mwaka 2013 umepanda
kulinganisha na mwaka 2012 ambapo waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka
la nne walikuwa ni 159,747 sawa na asilimia 43.08 huku waliopata sifuri
wakiwa 210,846 sawa na asilimia 56.92.
Watahiniwa wa shule
Dk Msonde alisema watahiniwa wa shule waliofaulu
mtihani huo ni 201, 152 sawa na asilimia 57.09 kati yao wasichana wakiwa
90,064 sawa na asilimia 55.49 na wavulana ni 111,088 sawa na asilimia
58.45.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea waliofanya
mtihani huo ni 34,075 sawa na asilimia 66.23 ya waliosajiliwa, wakati
2012, watahiniwa wa kujitegemea 26,193 walifanya mtihani huo.
Kuhusu mtihani wa maarifa (QT), Dk Msonde alisema waliofaulu mtihani huo ni 6,529 sawa na asilimia 43.38.
0 Comments