Sasa ni wazi
kwamba serikali mbili zimeonyeshwa taa za kijani baada ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kukamata uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba.
Jana kamati
14 za Bunge hilo ziliwachagua viongozi wake; Mwenyekiti na Makamu na 12
kati yake zilichukuliwa na wajumbe kutoka CCM, chama ambacho tayari
kimeweka wazi msimamo wake kuunga mkono Muungano kuwa ni serikali mbili.
Miongoni mwa
waliochaguliwa wenyeviti ni Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole
Sendeka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera na Uratibu), Steven Wassira
na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu ambao
wamekuwa mstari wa mbele kupigia chapuo mfumo huo badala ya serikali
tatu zinazopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba.
Wengine ni
Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango – Malecela, Naibu Spika wa Bunge
la Muungano, Job Ndugai, Mbunge wa Viti Maalumu, Kidawa Khamid Salehe,
Mbunge wa Kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha na Mbunge wa Mlalo, Hassan
Ngwilizi.
Wengine wa
CCM ni Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah na aliyewahi kuwa Waziri
katika serikali zilizopita Paul Kimiti. Pia wamo Mbunge wa Wawi ambaye
alifukuzwa uanachama na chama chake cha CUF, Hamad Rashid Mohamed na
Mwenyekiti wa kundi la wajumbe 201 wa kuteuliwa na Rais, Francis
Michael.
Katika
uchaguzi wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, aliyekuwa mwenyekiti wa
Muda na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho alichaguliwa
mwenyekiti na makamu wake, Dk Susan Kolimba.
Kamati ya
Uandishi wa Katiba ilimchagua Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge
na makamu wake, Mgeni Hassan Juma. Kwa kupata nafasi hizo ni dhahiri
kwamba ‘mapishi’ ya uendeshaji wa Bunge hilo yatafanywa na CCM kwani
mwenyekiti wake Samuel Sitta na makamu mwenyekiti Samia Suluhu Hassan
pia ni makada wa chama hicho.
Wenyeviti
hao wataungana na Sitta pamoja na Hassan kuunda Kamati ya Uongozi ya
Bunge Maalumu, ambayo ndiyo itakuwa na mamlaka ya kupanga ratiba na
miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa Bunge hilo.
Waliochaguliwa
kuwa makamu wenyeviti ni Profesa Makame Mbarawa, Shamsa Mwangunga,
Fatma Mussa Juma, Dk. Sira Ubwa Mamboya, Assumpter Mshama, Dk. Maua
Daftari na Waride Bakar Jabu. Wengine ni Biubwa Yahya Othaman, William
Ngeleja, Salimin Awadh Salimin, Yusuf Massauni na Thuwayba Kisasi.
Mbowe atimuliwa
Katika
uchaguzi huo, mjumbe wa Bunge hilo, Freeman Mbowe alitimuliwa katika
kamati alikokwenda kushiriki uchaguzi kwa madai kwamba hakuwa mjumbe.
Mbowe alisema kabla ya uchaguzi huo alimfuata Mwenyekiti Sitta kumwomba wafanye marekebisho katika kamati tatu za Bunge.
Alisema
waliafikiana kuwa Godbless Lema aliyekuwa Kamati namba saba ahamieKamati
namba mbili na AnnaMary Stella Mallac aliyekuwa Kamati namba mbili
ahamie Kamati namba sita.
Alisema kwa makubaliano hayo yeye (Mbowe) alihamia Kamati namba saba akitokea Kamati namba sita.
“Nilivyoingia
katika ukumbi wa Igada, wajumbe walianza kuguna mara wakaanza kuzozana
wakitaka wajumbe ambao hawakuwamo kwenye orodha ya kamati hiyo kutoka
nje,” alisema na kuongeza;
“Waliamua
kuitana majina, lakini hawakuona jina langu wakanitaka nitoke nje,
nikawaeleza makubaliano kati yangu na Mwenyekiti (Sitta) lakini
hawakuafiki walisisitiza nitoke ndani ya ukumbi huo.”
Alisema
hatua hiyo iliwafanya makatibu wasaidizi kuitwa na kuelezwa kilichotokea
ambapo waliwasiliana na Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Khamis Hemed
ambaye aliwajibu kuwa bado hajapokea taarifa za mabadiliko hayo na
kuwataka wasubiri awasiliane na Sitta.
“Wakati nikiendelea kusubiria
jibu, mmoja wa wajumbe aliendelea kupaza sauti akitaka niondolewe ili waweze kupiga kura,” alisema.
Alisema hali
hiyo ilimfanya yeye na baadhi ya wajumbe kutoka vyama vya upinzani,
akiwamo Profesa Abdallah Safari kususia uchaguzi huo na kuondoka.
Mbowe
alisema baada ya muda walifuatwa na makatibu wakiwaomba samahani warudi
ukumbini kwa sababu wamepokea maelezo kutoka kwa Sitta. Sitta
alithibitisha tukio hilo, lakini alisema halikuathiri matokeo ya
uchaguzi kwa sababu kuondoka kwao hakukuathiri akidi inayotakiwa.
0 Comments