WANANCHI TUTAUNGANIA NA (UKAWA) KUPATA KATIBA MPYA


Bunge Maalumu la Katiba sasa lipo katika hati hati ya kuendelea kutokana na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kutangaza kuwa hawatakuwa tayari kujadili rasimu tofauti na iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba bungeni.
Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana katika Ukumbi wa Pius Msekwa bungeni, viongozi wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, James Mbatia, Freeman Mbowe na Tundu Lissu, walisema wataitetea rasimu hiyo, ndani ya Bunge na kwenye Kamati.
“Rais Jakaya Kikwete amekuja bungeni siyo kufungua Bunge la Katiba bali kaja na mapendekezo ya rasimu ya CCM, sisi tutajadili rasimu ya wananchi ya Jaji Joseph Warioba ambayo inazungumzia muundo wa Muungano wa Serikali tatu,” alisema Profesa Lipumba.
Kutokana na msimamo huu wa Ukawa huenda Bunge litakwama kwani kwa mapendekezo ya CCM yenye Muundo wa Muungano wa Serikali mbili ni lazima kuandikwa upya Rasimu ya Katiba au kufanyika mabadiliko makubwa.
Profesa Lipumba alisema katika majadiliano juu ya rasimu, Ukawa watajikita kutumia Rasimu ya Katiba waliyopewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo imeeleza mapendekezo kwa nini yamefikiwa katika kila hoja,” alisema.
Hata hivyo, alisema wamesikitishwa sana na Rais Jakaya Kikwete, badala ya kufungua Bunge alijikita katika kuchambua rasimu na kuikosoa tume aliyoiunda mwenyewe.
“Rais Jakaya Kikwete siyo tu amemdhalilisha Jaji Warioba pamoja na wajumbe wa Tume, bali amewadhalilisha wananchi waliotoa maoni kwani hata takwimu alizotoa za kupinga rasimu siyo za kweli,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema muundo wa Serikali tatu ndio mawazo ya wananchi ambayo yamekusanywa na watu wenye heshma wakiwapo Jaji Warioba aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais na Jaji Augustino Ramadhani ambaye pia amewahi kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jaji Mkuu wa Zanzibar.
Alisema kauli za Rais badala ya kuimarisha umoja zimewagawa Watanzania kwani ametoa vitisho ambavyo havina sababu hasa kwa Wapemba bila kujua kuna Wanyamwezi wanaoishi Zanzibar.
Mbatia
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye pia ni mjumbe wa Bunge hilo, alisema kwa kauli ya juzi ya Rais Kikwete, kutangaza kuwapatia Zanzibar; watu, ardhi, mamlaka kamili na kusimamia uhusiano wa kimataifa ni kuvunja rasmi Muungano,
Mbatia alisema Rais Kikwete pia amewagawa Watanzania katika kauli zake ikiwa ni pamoja na ile ya Wapemba kwa kulima vitunguu katika Jimbo la Kibakwe kana kwamba ni makosa.
Alisema wamesikitishwa na Rais kuacha kufungua Bunge badala yake katumia taarifa potofu za mitaani kuligawa Bunge na kuwadhalilisha wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Hakuna asiyejua sasa tupo katika mgogoro mkubwa wa kikatiba, Zanzibar tayari ni nchi kamili kutokana na mabadiliko ya 10 ya katiba yao waliyoyafanya mwaka 2010 baada ya kupitisha dhana ya kuwa Zanzibar ni nchi,” alisema.
Mbowe
Mbowe alisema Rais amevunja maridhiano na hata kushindwa kusikiliza maoni ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Seneta Amos Wako kuwa maoni ya wananchi yaheshimiwe.
Alisema Serikali ya Kenya ilichakachua maoni, ilichakachua rasimu na kusababisha vurugu kubwa jambo ambalo linaweza kutokea kwa Tanzania.
“CCM wasijidanganye kwa wingi wao bungeni hakika katika hili tutatetea madai na maoni ya wananchi hadi mwisho,” alisema

0 Comments