MWENYEKITI WA KUDUMU BUNGE MAALUMU LA KATIBA KUPATIKANA LEO

Kamati ndio zitafanya kazi hivi kweli?

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu, Sitta alisema Viwango na Kasi ni sehemu ya maisha yake

Dodoma. Wakati Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta akichukua kwa mbwembwe fomu za kuwania nafasi ya uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba jana, wajumbe
wengine watatu nao wamejitokeza kuwania nafasi hiyo.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah, alilieleza gazeti hili kuwa, wajumbe waliojitokeza jana
hiyohiyo kuchukua fomu ni, Hashim Rungwe wa NCCR-Mageuzi, Dk Terezya Huvisa wa CCM na Mwenyekiti wa Chama cha Tadea, John Chipaka.
Wajumbe hao walichukua fomu hizo katika ofisi ya Katiba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana mchana, huku mchakato wa wake ukielezwa kuendelea hadi saa 4 asubuhi ya leo.
Sitta na Hashim Rungwe, walipatikana jana kuzungumzia hatua yao hiyo, lakini Chipaka na Dk. Huvisa hawakupatikana. Hata walipotafutwa kwa njia ya simu zao za mkononi,simu ziliita bila ya kujibiwa.
Mbwembwe za Sitta
Wakati wajumbe hao wakichukua fomu, Sitta alisambaza vipeperushi vya kuomba kura vikiwa na rangi za njano na bluu.
Katika kila ukurasa wa vipeperushi hivyo, ilielezwa kuwa atafanya kazi zote kwa viwango na kasi.
Katika vipeperushi hivyo, Sitta mwenye shahada ya sheria, anasema aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, aliyesimamia mabadiliko makubwa ya kanuni yaliyoimarisha uhuru na demokrasia ya Bunge.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu, alisema viwango na kasi ni sehemu ya maisha yake.
“Hata Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, nasimamia kwa kuzingatia viwango na kasi. Hata Bunge hili ukitaka utendaji bora lazima ufikie viwango vyake, ili yale unayoyafikiria yawafikie watu ndani ya wakati, siyo viwango bora huku shughuli hazimaliziki,”alisema.




Kuhusu tuhuma kuwa ni muumini wa Serikali tatu, Sitta alisema wakati alipokuwa akitangaza kuwania nafasi hiyo, walimwambia kuwa ni muumini wa Serikali tatu, lakini kauli hiyo haina ukweli.
Hata hivyo, alisema Serikali tatu ni namna ya kupanua wigo wa uongozi, ili watu walipane mishahara na kwamba kimsingi hakuna mahitaji ya Serikali tatu.
“Mimi si muumini wa Serikali tatu na nilichowahi kusema huko nyuma ni kwamba bila kutatua matatizo yaliyopo ndani ya Serikali mbili, mzigo wa Serikali tatu haubebeki,” alisema.
Hata hivyo, alisema sasa hawezi kuzungumzia suala hilo na kwamba anasubiri hoja zitakazotolewa katika mijadala ya Rasimu ya Katiba.
Kuhusu kuamua muundo wa upigaji wa kura, Sitta alisema kama atachaguliwa, atapokea ushauri kutoka katika Kamati ya Uongozi kuhusu jinsi ya kutatua jambo hilo lililowekwa kiporo katika kanuni.
Alisema kwa kutumia kamati hiyo hakuna jambo litakaloshindikana kupata suluhu, likiwamo suala la upigaji kura ambalo sasa linasubiri kamati ya kanuni itakayoundwa baadaye.
“Hii ni nafasi muhimu sana katika maisha yangu na ninatarajia kutumia uzoefu wangu na nguvu yangu, akili zote na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Kikubwa hapa itakuwa ni kuwezesha upatikanaji wa Katiba bora kwa wananchi. Tukishafanya hivyo basi nitakuwa nimeshamaliza kazi yangu,” alisema.
Taratibu za uchaguzi
Mapema, Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho, alisema uchaguzi wa mwenyekiti utafanyika leo jioni.
Alisema uchaguzi huo utafanyika baada ya wajumbe wanaotaka kuwania nafasi hiyo kuchukua fomu za kugombea.
“Wote wenye nia ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge, wanaombwa wakachukue fomu katika ofisi ya makatibu wetu, yaani Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Katibu wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar,” alisema.
Alisema fomu hizo zinatakiwa kurejeshwa saa 4.00 asubuhi katika ofisi za Bunge.
Kuhusu nafasi ya makamu mwenyekiti, alisema wanaotaka kuwania nafasi hiyo watachukua fomu baada ya kuchaguliwa kwa mwenyekiti na kusisitiza umuhimu wa makubaliano yaliyofikiwa kuhusu kuzingatia jinsia katika uongozi.
Kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa Bunge hilo, kila mgombea atatakiwa kujaza fomu na kuungwa mkono na wajumbe 20, 10 kutoka Tanzania Bara na 10 kutoka Zanzibar.
Kanuni hizo zinasema hakuna mgombea atakayeruhusiwa kujitoa katika kuwania nafasi hiyo baada ya uteuzi kufanyika.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, mwenyekiti na makamu wake, watachaguliwa kutoka miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa msingi kwamba kama mwenyekiti anatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi makamu wake atatoka upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano.
Aidha, sheria hiyo inasema uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti utaendeshwa kwa kura ya siri na mshindi atachaguliwa kutokana na wingi wa kura.
Pia mjumbe wa Bunge Maalumu, hatastahili kuteuliwa au kugombea nafasi ya kuwa mwenyekiti au makamu mwenyekiti isipokuwa awe amehitimu shahada kutoka katika chuo kikuu kinachotambulika.
Pia mgombea anatakiwa kuthibitisha kuwa ana uzoefu na ujuzi wa kuongoza mihadhara au mabaraza.
Pia awe hajawahi kutiwa hatiani na mahakama yoyote ya Jamhuri ya Muungano na kuhukumiwa
kifungu kisichozidi miezi sita kwa kosa lolote linalohusu kukosa uaminifu na maadili.
Rungwe naye atamba
Kwa upande wake, Rungwe aliyewahi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, alisema alikuwa na dhamira ya kuwania nafasi hiyo kwa muda mrefu, huku akiungwa mkono na wajumbe wengi kutoka vyama vya upinzani na baadhi kutoka kundi la wateule wa Rais.
“Nilikuwa na dhamira hiyo na wenzangu wameniomba nisimame. Vyama vyote vya upinzani vyenye wabunge na visivyokuwa na wabunge; NCCR-Mageuzi, CUF, Chadema, DP, Tadea NRA, TTP Maendeleo, UPDP, waliniomba niwawakilishe,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu uzoefu wake alijibu; “Nimewahi kugombea urais na niko mahakamani kila siku (kama wakili) na ni kiongozi wa chama.”
Kuhusu malengo yake, alisema anatarajia kusimamia muundo wa Muungano wa Serikali tatu na haki ya kumchagua kiongozi wa Tanganyika kama ilivyo kwa Wazanzibari wanaochagua Rais wao.
Alipoulizwa atawezaje kuwashawishi wajumbe wengine wanaoamini muundo wa Muungano wa Serikali mbili, alijibu kwa kusema: “Wanielewe kwamba nataka Serikali tatu, ya Muungano iwe ya Dola na zingine Serikali za Mitaa kama ilivyo Vatican.’

0 Comments