Nikiwa na Mh.Naibu Meya Prosper Msoffe, akinipa maelezo ya tukio na ushaidi wa kadi ya Hospitali na Dawa alizoandikiwa kutumia baada ya kipigo cha Mgambo wa Jiji la Arusha |
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.PICHA|MAKTABA |
Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amewashukia wajumbe wa Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliogomea kuendelea na mchakato wa kutengeneza Katiba, akisema wanapanga kuivuruga nchi.
Lukuvi alikwenda bungeni mjini Dodoma kwa kazi
maalumu ya kutoa ufafanuzi kuhusu kauli yake aliyoitoa kwenye Kanisa la
Methodist kwamba hoja ya serikali tatu ikipita inaweza kulifanya jeshi
kuchukua madaraka, ambayo imeibua hisia kali kutoka kwa wana Ukawa.
Akizungumza bila kuwapo wanachama wa Ukawa
waliosusia Bunge kuanzia juzi, Lukuvi alikishutumu Chama cha Wananchi
(CUF), kwamba kimekuwa kikijiita ni chama cha siasa wakati ni kundi la
Uamsho ambalo linasumbua Zanzibar.
Alisema kauli za Ukawa kwamba Rais Jakaya Kikwete
atapelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu The Hague, Uholanzi
haiwezi kutokea badala yake watakwenda wao katika mahakama hiyo kwa
kujihusisha na Uamsho.
Alisema ameamua kusema kile alichokichangia katika
kanisa hilo wakati wa kusimikwa kwa Askofu Joseph Bundala kwa kuwa hana
tabia ya unafiki na alitaka maneno hayo yarekodiwe kwenye kumbukumbu za
Bunge.
“Nayasema yote haya kwa kuwa naamini huo ndiyo
msimamo wangu na utakuwa msimamo ambao wakati wote utaendelea kuwa hivyo
na ninawataka ndugu zangu kuacha unafiki,” alisema.
Alikanusha madai kwamba ni mchokozi badala yake
akarusha tuhuma hizo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim
Seif Shariff Hamad.
Alinukuu hotuba ya kiongozi huyo wa chama kikuu
cha upinzani Zanzibar aliyoitoa mwezi uliopita katika Uwanja wa
Kibandamaiti Zanzibar kwamba imekuwa ikipotosha hotuba ya Rais Kiwete
kwa sehemu kubwa kuhusu mchakato mzima wa Katiba.
Lukuvi pia aliituhumu Ukawa kwamba imepanga
kuigawa Tanzania katika vipande, kwamba Zanzibar itatawaliwa na CUF,
Tanzania Bara na Chadema halafu CCM ipewe urais wa Muungano.
“Kutokana na hilo, nani ambaye hatakuwa na
wasiwasi juu ya haya mambo? Nataka niwahakikishieni katika Katiba hii
hakuna chombo chochote wala mtu yeyote atakayenizuia kusema
ninachokiamini ilimradi nasema ukweli na ninayoyaamini,” alisema.
Alisema kama maneno yake yamewachukiza zaidi
wapinzani, basi waendelee kugoma zaidi alichofanya kilikuwa kwenda
kusimamia masilahi ya serikali mbili zenye masilahi kwa wananchi.
Lukuvi alisema wakati wote wananchi hawataki
serikali tatu, bali wanataka maendeleo ikiwamo maji, barabara na vitu
vingine lakini vyote viwe kwa kupitishwa kwa serikali mbili.
Ampongeza Mrema
Waziri huyo alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mbunge
wa Vunjo na Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP),
Augustino Mrema kuhusu mchango wake bungeni juzi ambao uliunga mkono
muundo wa serikali mbili.
Lukuvi ambaye jana alimtaja Mrema kwa cheo cha
Naibu Waziri Mkuu alichowahi kushika katika Serikali ya Awamu ya Pili,
alisema mwanasiasa huyo ndiye mpinzani wa kweli ambaye anastahili
kupongezwa na kila mtu kwenye Bunge hilo kwa kuwa anachokizungumza ni
ukweli mtupu.
“Kutokana na hilo mheshimiwa Mrema, nakuhakikishia
kuwa sasa masilahi yako nitayafukuzia kwa sababu umeongea mambo ya
maana sana,” alisema Lukuvi.
Kwa muda mrefu Mrema amekuwa akifuatilia
serikalini kile anachokiita ni mafao na stahiki zake katika kazi ya
Unaibu Waziri Mkuu aliyoifanya wakati wa utawala wa Rais Mwinyi licha ya
kwamba nafasi hiyo haikuwamo kwenye katiba.
Akizungumza katika mkutano wa Ukawa jana,
Mwenyekiti Mwenza, Profesa Ibrahimu Lipumba alisema wanafanya taratibu
za kumchukulia hatua za kisheria Lukuvi kwa matamko aliyoyatoa.
“Alipaswa kusema kama kweli aliyazungumza maneno
yale au la na tungekuwa na uongozi unaowajibika baada ya kuyasema yale
(kanisani), Rais angemwita na kumtaka ayathibitishe,” alisema.
Alisema Uamsho ni taasisi ambayo imeandikishwa
kisheria na Serikali ya Zanzibar na kuongeza kuwa wakati inaandikishwa,
Chama cha CUF hakikuwa madarakani.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilikuwa haijaanza
Zanzibar, iliyouandikisha Uamsho ilikuwa Serikali ya CCM Zanzibar, sasa
hawaulizi kwa nini waliiandikisha?” alihoji Profesa Lipumba.
Alisema Uamsho wamekuwa wakimshambulia hata Makamu
wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad... “Huyu
tutamshughulikia kisheria kwa yale matamko aliyoyatoa,” alisema Profesa
Lipumba.
0 Comments