HOMA YA DENGUE INAHITAJI HATUA ZAIDI YA ELIMU

HALIMA MLACHA
HOFU na taharuki imewakumba wakazi wa jiji la Dar es Salaam, kutokana na kuzidi kuibuka kwa wagonjwa walioambukizwa virusi vya homa ya dengue, ambapo hadi sasa watu kadhaa wamepoteza maisha, wakiwemo wahudumu wa afya na madaktari.
Mpaka sasa ugonjwa huo hauna tiba maalumu wala chanjo; na njia pekee ya kukabiliana nao ni kutambua dalili zake, kama vile homa, kupungukiwa maji au damu, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu.
Dengue ni ugonjwa unaoenezwa na mbu aina ya Aedes na dalili hizi huanza kujitokeza kati ya siku ya 3 na 14, tangu mtu alipoambukizwa. Ugonjwa huo hauenezwi kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine, isipokuwa kupitia mbu huyo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ugonjwa huo ulianza kushambulia jiji hilo katika wilaya zake zote tatu za Ilala, Temeke na Kinondoni tangu Februari mwaka huu.
Kwa mara ya kwanza, ugonjwa huo uligundulika Dar es Salaam mwaka 2010, ambapo jumla ya wagonjwa 40 walithibitika kuambukizwa. Idadi ya waathirika iliongezeka na kufikia 172 kati ya Mei na Julai mwaka jana, ila hakuna aliyepoteza maisha.
Hata hivyo, tangu mlipuko huo ujitokeze mwaka huu, hali imezidi kuwa mbaya mwezi huu wa Mei, ambapo maambukizi ya virusi vya homa hiyo, vimezidi kuwashambulia watu wengi na wengine kupoteza maisha.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Kinondoni, Dk Gunini Kamba, amebainisha kuwa katika wilaya yake hadi sasa kuna wagonjwa takribani 100 wanaougua ugonjwa huo, wakati katika Manispaa ya Temeke wapo wagonjwa 15, kati yao tisa wakiwa ni wafanyakazi wa hospitali hiyo.
Kwa upande wake, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) yenyewe pekee imepokea wagonjwa 65 wanaosumbuliwa na ugonjwa huo. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, jiji hilo lote linakadiriwa kuwa na takribani wagonjwa 400 wa homa ya dengue.
Wakati idadi ya wagonjwa hao, ikizidi kuwachanganya madaktari hasa kutokana na ugonjwa huo kutokuwa na tiba, tayari zipo taarifa za watu takribani watatu wakiwemo muuguzi mmoja na daktari bingwa mmoja kupoteza maisha.
Kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo, kwa sasa ni kubwa, kutokana na ukweli kuwa bado elimu ya namna ya kudhibiti maambukizi yake haijafahamika; na kinachoendelea kwa sasa ni taharuki kwa wananchi, kwa kutojua nini cha kufanya.
Iko haja kwa mamlaka husika, kuanza kampeni mara moja kwa wananchi juu ya namna ya kuepukana na kuwadhibiti mbu hao, wanaoambukiza ugonjwa huo, hasa ikizingatiwa kuwa tabia yao tofauti na wale wa malaria, hung’ata mchana.
Wakati mamlaka hizo ikiwemo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, zikianzisha kampeni hizo, ikiwemo ya namna ya kuua mazalia ya mbu hao katika maeneo yote hatarishi jijini Dar es Salaam, pia yatolewe mafunzo kupitia Serikali za Mitaa ya namna ya kuwahudumia wagonjwa wanaokumbwa na ugonjwa huo.
Wengi wa wagonjwa waliopoteza maisha, sababu kubwa ni kuchelewa kuchukua hatua za kupambana na ugonjwa huo, kiasi cha kusababisha virusi hivyo kusambaa, lakini kwa wale wagonjwa waliowahi, wapo waliopona na kurejea katika kazi zao kama kawaida.
Elimu ya uhakika juu ya udhibiti wa maambukizi, lakini pia namna ya kuchukua tahadhari pindi mgonjwa anapopata ugonjwa huo, ndio silaha tosha ya kupambana na homa hiyo ya dengue, na kunusuru maisha ya wakazi wa jiji hilo, ambayo kwa sasa yako hatarini.

0 Comments