WATU sita wamefariki dunia papo hapo na zaidi ya 12 kujeruhiwa katika ajali mbaya iliyohusisha magari manne.
Akizungumzia tukio hilo lililotokea jana eneo la Makongo, jijini Dar
es Salaam, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura,
alisema kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya daladala inayofanya safari
kati ya Tegeta Nyuki na Ubungo lenye namba T 441 CKT, kuhama njia
kutokana na breki zake kushindwa kufanya kazi.
Kamanda Wambura alieleza kuwa baada ya daladala hiyo kuhama njia,
ilishia kuligonga daladala jingine lenye namba za usajili T 377 BEF aina
ya Nissan lililokuwa likitokea Makumbusho kwenda Kunduchi katika ubavu
wa kulia.
Alisema kuwa baada ya kugonga ubavuni, daladala hilo liliyumba na
kwenda kuligonga kwa nyuma gari jingine aina ya Toyota Discover lenye
namba za usajili T 454 AWZ.
Wambura alisema kuwa miili ya marehemu sita waliofariki ambao ni
wanawake watatu na wanaume watatu, imehifadhiwa katika Hospitali ya
Lugalo na majeruhi ambao ni wanaume nane na wanawake wanne wanaendelea
kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
Alisema kuwa dereva na kondakta waliokuwa kwenye gari ambalo lilisababisha ajali hiyo hawakupatikana.
0 Comments