LAANA YA WALIMU ITAIMALIZA SERIKALI HII


Mwl Daniel Urioh, Nikiwa mbuga ya Wanyama Arusha, walaokujipumzisha kidogo kutokana na kupuuzwa sna na taifa langu Tanzania. Niwakati muhafaka sasa taifa kulipa waalimu vizuri na kuwawezeshwa zaidi kiuchumi, ndipo mtaona ubora wa elimu ukishamiri.
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda alinukuliwa bungeni Alhamisi iliyopita akisema; “Sasa ni faraja kwa walimu, maana juzi tulikaa katika Baraza la Mawaziri na tumekubali kuanzisha chombo maalumu kitakachoshughulika na nidhamu na ajira za walimu, tunaamini masuala yao yote yatapatiwa ufumbuzi…”

Tunaona haraka kuwa kutakuwa na chombo (baraza, tume, kamati) ambacho kitashughulika na nidhamu. Hii ni nidhamu ya nani? Ya walimu au ya serikali na watumishi wake? Kwa serikali, neno nidhamu lina maana gani hasa? Serikali inashughulikiaje nidhamu? Uzoefu unatuelekeza wapi pale serikali inapozungumzia nidhamu?
Tayari Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu (CWT), Ezekiel Oluoch, amesema chombo hicho ni muhimu kwani kitasimamia kazi tano: Kuajiri, kulipa mishahara, kuangalia mahitaji ya walimu, kupandisha vyeo walimu na kufukuza walimu.
Hapa inawezekana “kufukuza walimu” ndiyo sehemu ya nidhamu. Uzoefu wa matumizi ya neno “nidhamu” katika mahusiano na serikali umekuwa ni kuonya, kukaripia, kukemea, kusuta, kuadhibu, kusimamisha kazi, kufukuza kazi na lolote linaloonyesha mabavu ya muhusika kwa yule aliye chini yake.
Nidhamu kwa maana ya serikali na uzoefu, ni kuzuia walimu kugoma; kuzuia walimu kulalamika hadharani na katika vyombo vya habari (lazima wafe kiofisa!); kuzuia walimu kudai haki zao nje ya utaratibu uliowekwa na ambao sharti uwe sambamba na matakwa ya serikali.
Nidhamu ya serikali yaweza kuwa ni kusubiri, bila “kuulizauliza” juu ya makato kwenye mshahara wako; kutolipwa mshahara stahiki; kutopandishwa ngazi wakati unapowadia; kutodai nyongeza, gharama za usafiri unapohama; posho ya kujikimu unaposafiri; nyumba ya kuishi mahali penye mazingira magumu.
Nidhamu yaweza kuwa amri ya kukaa kimya pale unapodai serikali iliyolimbikiza madeni yatokanayo na kutokulipa mishahara na posho.
Kwanini tufikirie hivyo? Jibu ni swali jingine. Kwani serikali imekuwa inashindwa nini na vipi kulipa walimu – mishahara na marupurupu yao? Kwani “chombo” kitapata wapi fedha hizo? Au tuseme sasa kwamba serikali itakuwa imepumzika – kero zote zitahamishiwa kwenye chombo ambacho kitakuwa na mamlaka ya kuchukua “hatua za kinidhamu?”
Bunge linaketi, linajadili na kupitisha bajeti. Mafungu yanaonekana. Fedha hazipelekwi. Taasisi, asasi au ofisi husika inabaki kuuma vidole. Inabakiwa na kazi moja tu – ile ya “kutunza nidhamu” kwa mujibu wa mahitaji na uzoefu wa serikali – kunyamazisha wanaodai, wanaolalamika, wanaonung’unika, wanaopinga na wanaotaka kuandamana.
Siyo busara sana kuanza kushangilia kuwepo kwa chombo hata kabla hakijaundwa na kuona mfumo wake na wahusika. Shetani ana tabia ya kujiremba kwa nguo, marashi na kauli!
Faraja inayotajwa na waziri mkuu ni faraja iliyoahidiwa na Baraza la Mawaziri. Hili baraza ni lilelile ambalo limekuwepo likifanya yaleyale ambayo walimu wamekuwa wakipinga, wakilalamikia, wakijutia. Ni baraza linalotaka kazi yake ichukuliwe na mwingine na aifanye kama ambavyo limekuwa likisimamia na hata kung’ang’ania.
Inawezekana ujio wa “chombo” usiwe faraja. Inawezekana ukawa karaha. Ukawa laana. Ukawa maafa. Tusubiri.

0 Comments