Kwa ufupi
- Alimshikia mama yake kisu akilazimisha apewe fedha za kununulia dawa za kulevya. Siku nyingine alimnyonga mkono kumpora simu akauze.
Pamoja na mambo mengine kwenye eneo hilo,
walikuwapo watu wawili ambao walitoa ushuhuda wa madhara ya dawa za
kulevya kwa binadamu na jamii kwa ujumla na kusababisha watu waliokuwapo
kukumbwa na baridi ya woga kama mbwa aliyeona chatu.
Mashuhuda hao ambao walisafirisha, walitumia kwa
njia mbalimbali dawa za kulevya na hatimaye kujinusuru ni Very Fidelis
Kunambi na Rehema Chalamila maarufu kwa jina la Ray C.
Hata hivyo aliyewaliza wengi na kuwafanya
wafikirie mengi ni Ray C ambaye leo tunalazimika kukuleta kauli yake
yote akianza hivi,
“Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kuniwezesha kuwa hapa leo nikiwa mzima mwenye afya na moyo wa ujasiri.
Natumia fursa hii pia kuwashukuru Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za
Kulevya kwa kunialika kutoa ushuhuda wangu. Nafurahi kwa mahudhurio haya
ya viongozi na wananchi, Nawapenda wote.
Naitwa Rehema Chalamila, wengi wananifahamu kwa
jina la Kisanii la “Ray C”. Mungu alinibariki na kuwa mtu mwenye
mafanikio makubwa kwani nikiwa na umri wa miaka 17 nilifanikiwa kupata
kazi ya utangazaji katika Radio East Africa, mwaka 1999, mwaka 2000
nilijiunga na Radio Clouds. Mafanikio yangu hayakuishia hapo, nikiwa
Radio Clouds mwaka 2002 nilianza muziki na kupata mafanikio makubwa
sana. Mafanikio ambayo yaliniwezesha kujenga nyumba nzuri na kubwa
nikiwa na umri wa miaka 19, baadaye kununua magari na kufungua maduka
makubwa jijini Dar es Salaam na hatimaye kuwa msaada mkubwa wa familia
yetu.
Aidha, nilitembelea Marekani, Dubai, Sweden,
Hongkong, Uganda, Kenya, Afrika Kusini, , Uingereza, China, Oman,
Australia, China, Norway, Msumbiji, Afrika Kusini, India, na Nigeria
kufanya muziki.
Dawa zamgeuza miguu juu kichwa chini
Ghafla ujana ulionipaisha na kunipeleka juu
ukanigeuza kichwa chini miguu juu. Nuru na nyota yangu ikafifia, Nikawa
sionekani kiasi cha watu wakafikia kusema nimekufa.
Uwezo wangu wa kufanya muziki ulitoweka, nilianza
kuuza vitu vyangu kimoja baada ya kingine nikianza na vidogo vidogo,
mwisho nikauza magari yangu, Nyumba nayo ikaenda, Maduka nayo
nikayafilisi nikafunga, nikaanza kuwa mtu wa kujificha huku nikendelea
kudhoofika.
Ilifika wakati nililazimika kutembea nimevaa
“kininja”. Mungu wangu! Nilikuwa nimenasa kwenye mdomo wa mamba, dawa za
kulevya zilikuwa zinanimaliza! Nilipokuja kushtuka nilikuwa tayari
nimenasa, Maisha yangu yakawa si starehe tena bali mateso na aibu!
Nilipokuwa katika uteja nilikwenda mbali zaidi ya
kuuza vitu vyangu vya thamani. Roho inaniuma sana ninapokumbuka
nilipomshikia kisu mama yangu mzazi kumlazimisha anipe hela nikanunue
dawa. Roho inaniuma sana ninapokumbuka nilipomnyonga mkono mama
kumpokonya simu.. ninapokumbuka haya roho huwa inaniuma kuliko hata
kupoteza vitu vyangu vya thamani nilivyopoteza.
Namshukuru mama alitambua sikuwa mimi, hakunikatia tamaa
aliendelea kunihangaikia na kufanya maombi sana. Samahani kwa mateso
niliyokupa na asante sana mama yangu, Mungu azidi kukubariki. Nawaomba
wazazi Chonde Chonde wasaidieni vijana wenu.
Mheshimiwa, nakumbuka nilivyofukuzwa kama mbwa kwa
muuza dawa kwa sababu nilikuwa sina hela, naumia sana ninapokumbuka
siku nilizokuwa nalala kwenye boksi, siwezi kurudi nyumbani nikiwa arosto.
Kwa sababu ya kukosa dawa kwa kukosa hela nikalazimika kulala kwenye
boksi kusubiri labda itatokea “kampani” ininunulie dawa nipone. Yalikuwa
ni mateso ya ajabu ambayo hayana mfano.
Azungumzia familia nzima ilivyoteseka kwake
Mateso na dharau nilizopata hazikuwa zangu peke
yangu. Familia yangu pia ilikuwa katika dimbwi la mateso, Familia yote
iliumwa, mama yangu alilia sana na kuhaangaika... mwanangu...nini
hiki... umerogwa na nani mwanangu? ... ee Mungu nisaidie. Kilikuwa
ndiyo kilio cha mama kila wakati. Mtu aliyekuwa akitegemewa na familia
nilikuwa natoweka taratibu .. sasa nikawa mzigo mkubwa kwa familia.
Nilikuwa naumia sana na nataka kuacha lakini
nimenasa kwenye meno makali ya mamba sina ujanja. Mama alihangaika sana
na ndugu zangu pia walikosa raha. Mama alikuwa ni mtu wa kwenda kwenye
maombi kila wakati. Alikuwa na fedha lakini naye uchumi wake uliporomoka
na kutoweka kwa sababu yangu mimi.
Mungu ameonyesha nguvu zake
Hatimaye Mungu alimwinua Mheshimiwa Rais Jakaya
Mrisho Kikwete na kunisaidia kwa kunipa matibabu na kwa sababu nilikuwa
na dhamira ya kuacha, kwangu ilikuwa ni jambo rahisi kuachana na dawa za
kulevya.
Nitumie fursa hii kwa mara nyingine kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa nyingine ya kuwa Ray C, lakini siyo tu
kuwa Ray C yuleyule wa zamani, bali kuwa Ray C mwenye akili na mitazamo
mipya kabisa ya maisha na ambaye Watanzania na taifa litanufaika naye
sana!
Ampigia magoti JK
Kwa namna ya kipekee kwa mara nyingine namshukuru
sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Kikwete kwa
kunisaidia Mungu azidi kumbariki. Ninaahidi leo, kwa kunisaidia mimi
wengi watapona!
Na najua hiyo ndiyo ilikuwa dhamira yake, niwe
mfano ili wengi waokoke na janga hili. Na Ninaamini Mungu alikuwa na
mpango na mimi, lazima nimtumikie kwa njia hii.
Ataja siri za kutumia dawa za kulevya
Kilichoniingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya ilikuwa ni
marafiki wabaya na mahusiano mabaya ya kimapenzi, ambapo kupitia mtu
niliyempenda na kumwamini sana katika mazingira ambayo hayakuwa wazi
nilijikuta nimeshanasa kwenye matumizi ya dawa za kulevya.
Nilipokuwa katika tatizo hilo nilijifunza mambo
makubwa matatu, jambo la kwanza ni kuwa siyo wote wanaotumia dawa za
kulevya wameingia huko wakijielewa.
Pili kuna unyanyapaa mkubwa wanaofanyiwa
waathirika wa dawa za kulevya kutoka kwa jamii na vyombo vya dola, na
kwa asilimia kubwa unyanyapaa huo unatokana na uelewa mdogo wa jamii na
vyombo vya dola juu ya hali halisi ya tatizo.
Tatu, nilijifunza kuwa watu kuendelea kutumia dawa
hizi na tabia nyingi hatarishi wanazokuwa nazo hakutokani na wao
kupenda bali mateso makali ambayo mtu anayapata anapokosa dawa hizo.
Roho inaniuma sana ninapowaona waathirika wa dawa
kwenye maskani zao au popote, najua mateso mazito waliyonayo tofauti na
jamii inavyofikiri.
Sasa kuongoza vita dhidi ya dawa za kulevya
Kutokana na Mungu kunisaidia kwa kumtumia Dk
Jakaya Mrisho Kikwete, na jinsi mimi mwenyewe ninavyoguswa na tatizo
hili, shukrani yangu kubwa kwa Mwenyezi Mungu na Mheshimiwa
Rais Kikwete ni kufanya juhudi kuelimisha jamii
juu ya athari za dawa za kulevya. na pia kuwasaidia waliokwishaingia
watoke na ambao hawajaingia wasithubutu.
Kwa kufanikisha hilo nimeamua kuanzisha asasi
inayoitwa Ray C Foundation, asasi hii ina lengo la kufanya uelimishaji
mkubwa kwa jamii kupitia makundi yake mbalimbali pamoja na kusaidia
walioathirika warudi kuwa watu wa kawaida,
Kwa kupitia Ray C Foundation tayari tumeanza
kampeni ya shule kwa shule tukitembelea baadhi ya shule za sekondari
za jijini Dar es Salaam, na tuna lengo la kuzitembelea shule zote za
sekondari katika mikoa yote ya Tanzania hasa ile iliyoathirika zaidi na
dawa za kulevya.
Vile vile tumeanza kutembelea vijana watumiaji
dawa za kulevya kwenye maskani zao na kuwaelemisha waache na katika
miezi miwili tu ya kampeni hiyo vijana 25 wameamua kuacha na sasa
wanapata matibabu ya Methodone.
Aidha, tunakusudia kufanya uelimishaji kwa makundi mbali mbali ya kijamii kwa kutumia njia mbalimbali.
0 Comments