MARUFUKU KULIPA ADA VYUO VIKUU KWA DOLA

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imepiga marufuku vyuo vikuu kutoza ada kwa dola kwa wanafunzi Watanzania wanaosoma katika vyuo hivyo.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni mjini hapa jana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenister Mhagama alipojibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kisangi (CCM).
Kisangi alitaka kujua tamko la serikali kuhusiana na ada kubwa inayotozwa kwa dola za Marekani kwa baadhi ya vyuo vikuu nchini. 
Akiendelea kujibu, Mhagama alisema serikali kupitia Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) itaendelea kusimamia utekelezaji wa mwongozo wa ada elekezi ili kudhibiti utoaji wa ada usiozingatia hali halisi ya gharama za uendeshaji.
 “Kutoza ada kwa dola ni kinyume na taratibu, vyuo vikuu vizingatie agizo la serikali la kutoza ada kwa fedha za Kitanzania,” alisema. 
Katika swali la msingi, mbunge huyo alihoji mpango wa serikali wa kupunguza gharama za masomo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ikizingatiwa kuwa vyuo vinazidi kuwa vingi.
  “Gharama za masomo katika vyuo vikuu nchini imezidi kuwa kubwa hasa kwa wanafunzi ambao hawapati mkopo, mzigo mkubwa unakuwa kwa wazazi wao,” alisema mbunge huyo.
Naibu Waziri alikiri ada za masomo zimetofautiana kati ya chuo kimoja na kingine na kati ya programu moja na nyingine.
 “Ili kupunguza tatizo hilo, serikali mwaka 1994 ilianzisha utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu wakiwemo wenye uhitaji,” alisema. 
Sambamba na hilo alieleza kuwa mwaka 2004, serikali ilianzisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa sheria namba 9 ili kuimarisha utaratibu wa kutoa mikopo hiyo.

0 Comments