Kwa ufupi
- Mkakati wa kubana matumizi kuumiza wengi serikalini
- Ushuru wa soda, juisi, bia, mvinyo, vinywaji vikali na sigara waongezeka
- Umri wa uchakavu wa magari yanayotozwa asilimia 25 wapunguzwa kutoka miaka 10 hadi minane
Kinyume na bajeti ya mwaka jana
iliyoonekana ni ‘majanga’ kwa kila eneo, mwaka huu Serikali imetoa ahadi
za kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma katika ununuzi na
misamaha ya kodi ili kuhakikisha fedha hizo zinaelekezwa kwenye shughuli
muhimu za maendeleo na huduma za jamii.
Hayo yamo katika hotuba ya Bajeti iliyosomwa bungeni, Dodoma jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum.
Hata hivyo, uamuzi huo kama njia
ya kupate fedha zaidi umeelezwa kuwa ni ‘mzuri wenye tatizo la jinsi
gani ya kupima utekelezaji wake’.
Mhadhiri wa Shule ya Biashara ya
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Goodluck Urassa alisema kuna matatizo
makubwa ya uwajibikaji yanayoweza kuzorotesha nia njema ya kubana
matumizi na kudhibiti misamaha ya kodi.
Pia, katika hotuba hiyo kilio
cha muda mrefu cha wafanyakazi kutaka kupunguziwa kodi kwenye mshahara
hadi chini ya asilimia 10, kimeendelea kuwa kitendawili baada ya
Serikali kupunguza kwa asilimia moja tu, kutoka 13 hadi 12 huku Kima cha
Chini cha Mshahara (KCC), kikielezwa kwamba kitaongezwa lakini bila
kuwekwa wazi kwa kiwango gani.
Hotuba hiyo pia haikubainisha
vyanzo vipya vya mapato vilivyoainishwa, suala ambalo awali, lilizua
mvutano mkali kati ya Serikali na Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Badala yake, imeendelea na utamaduni uleule wa kuzikamua kodi bidhaa zilezile zikiwamo soda, pombe, sigara na magari.
Hata hivyo, Waziri Mkuya alisema
Bajeti yake imelenga kupunguza gharama za maisha ya wananchi kwa
kuendelea na jitihada za kudhibiti na kupunguza mfumuko wa bei,
kuboresha huduma za jamii, miundombinu ya barabara, umeme na
umwagiliaji.
Kudhibiti matumizi
Mkakati kabambe aliokuja nao
Waziri Mkuya ni wa kuimarisha zaidi usimamizi na udhibiti wa matumizi ya
fedha za umma, kuongeza nidhamu ya matumizi na uwajibikaji kwa wadau
wote wanaotekeleza Bajeti ya Serikali.
Pengine jambo muhimu katika
mkakati huo ni kuunganisha matumizi yote ya Serikali, yaani wizara,
idara za Serikali zinazojitegemea, sekretarieti za mikoa, mamlaka za
Serikali za mitaa na wakala na taasisi za Serikali chini ya mfumo mmoja
wa udhibiti wa fedha za umma unaosimamiwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali.
Katika kutekeleza hilo, kuanzia sasa hakuna
taasisi yoyote ya umma inayokusanya maduhuli itakayoruhusiwa kutumia
fedha walizokusanya kabla ya bajeti yao kupitiwa na kuidhinishwa na
Mlipaji Mkuu wa Serikali na fedha zote zinazozidi bajeti iliyoidhinishwa
zitawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
“Utaratibu huu unatumiwa na nchi
nyingine duniani zikiwamo nchi jirani na kwa hapa Tanzania utaratibu
huu unatumika kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania,” alisema Waziri Mkuya.
Ili kuondoa tatizo la
utekelezaji wa miradi ya chini ya viwango, Serikali imenunua vifaa vya
kuhakiki ubora wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha kuwa thamani ya
fedha inawiana na uwekezaji katika miradi husika na kuwabaini
makandarasi dhaifu katika ujenzi wa miundombinu na kuwachukulia hatua.
Vile vile Waziri wa Fedha
alitangaza mpango wa Serikali wa kufanya ununuzi wa pamoja (bulk
procurement) kutoka kwa wazalishaji badala ya kutumia wakala kama ilivyo
sasa na hatua imeanza kuchukuliwa ili ununuzi wa magari na vyombo vya
Tehama ufuate utaratibu huo.
Alisema katika mwaka ujao,
vitabu vya kumbukumbu (diaries) na kalenda za kila mwaka, zitachapishwa
na Ofisi ya Waziri Mkuu tu na kuondokana na utaratibu wa sasa wa wizara,
idara zinazojitegemea, wakala na taasisi za Serikali, mikoa na mamlaka
za Serikali za Mitaa kila moja kuchapisha kwa utaratibu wake.
Ukiacha eneo la matumizi, waziri
alisema Serikiali inalenga kuongeza mishahara ya watumishi wa umma,
kuendelea kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, kuongeza fursa za
ajira na kuimarisha utawala bora.
Kuhusu Kodi
Waziri huyo alisema kodi katika
vinywaji baridi, ushuru kwenye maji ya matunda (juisi), mvinyo na sigara
vinatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh124, 2 milioni.
Katika magari, Serikali
inatarajiwa kuongeza kodi kwa yale yatakayoingizwa nchini yakiwa
yametumika kwa zaidi ya miaka minane baada ya kubadilisha ukomo wa umri
wa magari yasiyo ya uzalishaji (non-utility vehicles) na magari ya
uzalishaji na yasiyobeba abiria (non-passanger utility vehicles), kutoka
miaka 10 hadi minane.
Katika suala la misamaha ya kodi
ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi na wabunge, Waziri Mkuya
aliainisha baadhi ya mabadiliko katika Sheria ya Kodi na Uwekezaji
yakiwamo ya kuondoa saruji katika orodha ya bidhaa zinazofikiriwa kuwa
za mtaji, kufuta misamaha ya kodi iliyokuwa inatolewa kwa kampuni za
simu, kuongeza mtaji wa wawekezaji wanaotoka nje kutoka Dola za Marekani
20 milioni hadi Dola 50 milioni.
0 Comments