MADUDU VITABU VILIVYONUNULIWA KWA CHENJI YA RADA

Mbunge wa kuteuliwa na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, Mh. James Mbatia. Mwanasiasa huyu amekuwa mstari wa mbele kuikosoa serikali kwa kupitisha na kusambaza vitabu vyenye makosa shuleni.
Kwa ufupi
Juni mwaka jana, Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha NCCR- Mageuzi na mbunge wa kuteuliwa na Rais, aliweka bayana udhaifu mwingi aliogundua kuwemo katika vitabu vilivyoidhinishwa na iliyokuwa Kamati ya Ithibati ya Vifaa vya Elimu
Pamoja na kelele nyingi za wabunge wakiongozwa na James Mbatia kuhusu udhibiti wa vitabu vinavyotumika shuleni, kuna kila dalili kuwa watendaji wa vyombo husika wameweka nta masikioni.Juni mwaka jana, Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha NCCR- Mageuzi na mbunge wa kuteuliwa na Rais, aliweka bayana udhaifu mwingi aliogundua kuwemo katika vitabu vilivyoidhinishwa na iliyokuwa Kamati ya Ithibati ya Vifaa vya Elimu (EMAC).
Madudu vitabuni
Japo kilio chake kilichoungwa mkono na wabunge wengi kilisikika kwa uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuamua kuivunja (EMAC), madudu zaidi yamebainika kwenye vitabu vilivyonunuliwa kwa fedha za fidia ya rada na kusambazwa shuleni.Mwaka jana, serikali ilitangaza kuwa fedha hizo ambazo ni Pauni 29.5 milioni za Kiingereza (sawa na Sh73.6 bilioni), zililengwa kwa ajili ya ununuzi wa vitabu vya kiada, mihutasari ya elimu ya msingi na madawati.Ukiondoa mgawanyo wa vitabu hivyo ambavyo haukuzingatia mahitaji kwa shule, walimu katika maeneo mbalimbali nchini wanalalamika kuwa vitabu vingi vina makosa ya maarifa na uchapaji, licha ya kuwa vilipata ithibati kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Mifano ya makosa
Kitabu kimoja cha hisabati darasa la saba, kuna tofauti ya majibu ya maswali namba 7 na 12 kama yalivyo katika kitabu chake cha Kiongozi cha Mwalimu. Swali la 7 (-17 ×-13) ambalo jibu lilipaswa kuwa +221, mwandishi ameweka jibu la +909903391 ambalo ni jibu la swali la 12 linalosema: -31375979× -29
Katika kitabu hichohicho, kuna swali linalosema; Tafuta kipeuo cha pili cha 102 - 62 , badala jibu kuwa 8 mwandishi ameandika 20
Aidha, katika mada ya Ubongo wa Nyuma (serebelamu), kitabu kimoja kinasema serebelamu huhusika na matendo yasiyo ya hiari huku kitabu kingine kikielezea kuwa serebelamu inahusika na uratibu wa matendo ya hiari.
Kasoro nyingine imejitokeza katika tofauti ya majina na idadi ya aina za misuli. Kitabu kimoja kinaaandika kuwa kuna aina kuu mbili za misuli katika mwili wa binadamu ambazo ni misuli ya hiari na misuli isiyo ya hiari huku kingine kikisema kuna misuli mikuu ya aina tatu ambayo ni misuli myoyoro, misuli ya moyo na misuli ya mfumo wa mifupa.
Kitabu kingine cha Kiswahili, mwandishi amekosa mtiririko wa kiuandishi hivyo kuwakanganya walimu na wanafunzi wanaokisoma. Katika kitabu hicho mada ya Aina za Maneno iliyoanza ukurasa wa 10 na aina ya kwanza ‘Nomino’ badala ya kuendelea na mada hiyo kwa mfuatano wa kurasa, aina nyingine na manezo zinaonyeshwa kutajwa ukurasa wa 85 na 118.
Kauli ya msomiDk George Kahangwa, mtaalamu wa fani ya elimu na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anaona mambo hayo ni aibu kwa taifa.
“Haya ni miongoni mwa mambo yanayoliaibisha taifa letu na kulitengenezea kifo cha taratibu. Itakumbukwa kwamba hii si mara ya kwanza tunasikia uwepo wa aibu hii ya vitabu vibovu. Itakumbukwa kwamba katikati ya mwaka jana, Taasisi ya EMAC ilishutumiwa bungeni kwa kutoa ithibati kwa vitabu visivyo na viwango, hadi serikali ikaamua kuifuta taasisi hiyo.
Ilielezwa bungeni kwamba huenda ufisadi ulichangia kupitishwa kwa vitabu hivyo. Si ajabu hata mara hii ufisadi (kwa maana ya rushwa) una mkono wake katika kununuliwa, kuthibitishwa na kuidhinishwa matumizi ya vitabu hivi visivyofaa.Hata hivyo, kama taifa, tumefika hapa si kwa sababu tu ya rushwa bali mzizi wa tatizo ni watu kukosa uzalendo, umakini na uelewa wa wanachokifanya.
Aidha, uzembe uliokithiri miongoni mwa viongozi na maofisa husika unachangia sana. Ofisa mwenye uzalendo hawezi kutanguliza masilahi yake ya kupata chochote, ilihali anatoa ithibati kwa ajili ya vitabu vitakavyoangamiza elimu katika taifa lake.Ofisa makini hawezi kuruhusu kitu kisicho na viwango kupite mikononi mwake kwenda kuwadhuru walaji.Mjuzi wa kazi anayoifanya ni mwepesi wa kuona mushkeli katika kaziiliyofanyika na kuzuia isitumike.
Katika taifa letu imekuwa ni kawaida kukuta nafasi nyingi za kazi nyeti zinazohitaji wataalamu wa fani husika, wamepewa watu wasio na ujuzi katika fani hiyo. Matokeo yake ndiyo haya.Katika hili, serikali inao wajibu wa kufanya kazi zake kwa uangalifu mkubwa. Kama vile kampuni zinazotengeneza magari zinapogundua modeli fulani ya gari iliyosambazwa kwa watumiaji imekosewa, hutoa wito wa kuirejesha kiwandani kutoka pembe zote za dunia, ndivyo na serikali yetu inavyopaswa kufanya kuhusu vitabu hivi.
Kama vile serikali yetu ilivyolazimika kuwawajibisha wafanyakazi wa EMAC, ndivyo inavyopaswa kuwashughulikia wahusika katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na idara nyinginezo zilizohusika katika hili.


0 Comments