Mh Shukuru Kawambwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi |
Kwa ufupi
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Iyunga ya
jijini hapa, France Mung’ong’o alisema jana kuwa yeye pamoja na
wafanyakazi wa shule yake wameshikwa na ganzi kutokana shule yake kuwa
moja ya shule 10 za mwisho kwa matokeo mabaya.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Iyunga ya
jijini hapa, France Mung’ong’o alisema jana kuwa yeye pamoja na
wafanyakazi wa shule yake wameshikwa na ganzi kutokana shule yake kuwa
moja ya shule 10 za mwisho kwa matokeo mabaya.
“I’ m shocked (nimeshtushwa). Sikutarajia matokeo
haya. Si mimi tu, hata walimu wenzangu hadi sasa hawaamini kwani kwenye
mtihani wa mock (majaribio) ya kitaifa wanafunzi wangu walifanya vizuri
na wa daraja la kwanza walipatikana wanafunzi 14 kipindi hicho,’’
alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, walimu jana
walikuwa na vikao vya kiidara na leo wanatarajia kufanya mkutano wa
pamoja kusaka sababu za kufanya vibaya.
Wanafunzi ambao sasa ni wa kidato cha sita walipoulizwa jana kuhusu habari hizo walijibu kwa sauti kubwa ‘mbayaaa’.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa juzi Shule ya
Sekondari ya Iyunga iliyoanza 1960, ni ya 262 kati ya sekondari 268 za
aina yake kitaifa jambo lililoifanya iwe moja ya shule 10 za mwisho.
Akizungumza jana baada ya kuulizwa sababu za shule
hiyo kufanya vibaya, Mng’ong’o alisema: “Nimeshikwa bumbuazi kutokana
na ukweli kwamba nilikuwa nikiamini kwamba mwenendo wa kitaaluma
unapanda.”
Hata hivyo alisema kero za jumla ambazo anahisi
kuchangia ni upungufu wa walimu na wanafunzi wengi kurundikana kwenye
darasa moja .
Alisema kwa kawaida shule yake ni ya mchepuo wa
sayansi na kwamba ni makosa wanafunzi zaidi ya 100 kukaa chumba kimoja
kufundishwa masomo ya Fizikia, Baiolojia na Kemia.
“Pia shule yangu ina upungufu wa walimu sita wa kidato cha tano na sita. Hivi sasa wapo walimu 11.
Mwalimu wa taaluma, Muhoja Bundala akitoa maoni
yake alisema watakaa kuchambua sababu na kwamba hawatakubali kushika
mkia mwakani.
Bundala aliwataka walimu na wanafunzi wa shule
hiyo kuwa watulivu katika kipindi hiki wakati wakitafakari na kwamba
kinachotakiwa ni kujipanga.Akizungumzia jana, mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari Tambaza,
Hussein Mavumba alisema kuwa wameyapokea matokeo hayo kwa mshtuko mkubwa
kwani halikuwa jambo walilokuwa wakilitarajia.
Mwalimu Mavumba alisema kuwa amewaita walimu na
baadhi wa wakuu wa idara za masomo kuona nini kimetokea hata shule hiyo
iliyokuwa maarufu kwa kufanya vizuri kushika nafasi 10 za mwisho.
“Nitakutana na walimu wangu na tutafanya tathmini za kisayansi kujua nini kilikosewa hadi kusababisha matokeo hayo,” alisema.
Baadhi ya wanafunzi walioomba kutokutajwa majina
yao, waliidokeza Mwananchi kuwa uhaba wa walimu masomo ya sayansi ambayo
ndio yameongoza kwa kufelisha zaidi shuleni hapo, upungufu wa vifaa vya
maabara na uzembe wa wanafunzi wenyewe ni miongoni mwa sababu
zilizochangia matokeo mabaya.
Shule ya Sekondari Tambaza imeshika nafasi ya tatu
kutoka mwisho, matokeo mabaya zaidi yakilinganishwa na yale ya miaka
minne iliyopita.
Imeandikwa na Lauden Mwambona na Mosha Mustapha, IJMC.
0 Comments