Wanafunzi wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari ya wavulana mchepuo
wa Sayansi ya Iyunga ya Jijini Mbeya, wakiwa wamesomangana katika chumba
kimoja wakati wa masomo yao jana asubuhi. Mkuu wa Shule hiyo France
Mng'ong'o, alisema kuwa kidato kimoja kina wanafunzi zaidi ya 100 na
kutokana na upungufu wa walimu wanalazimika kusongamana ndani ya chumba
kimoja kwa lengo la kumsikiliza mwalimu wa somo husika.
Kwa ufupi
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wadau hao
walisema pamoja na matokeo hayo kuonyesha ongezeko la ufaulu, wana
wasiwasi iwapo matokeo yaliyoandikwa kwenye karatasi yanaakisi ufahamu
wa wanafunzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wadau hao
walisema pamoja na matokeo hayo kuonyesha ongezeko la ufaulu, wana
wasiwasi iwapo matokeo yaliyoandikwa kwenye karatasi yanaakisi ufahamu
wa wanafunzi.
Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Susan Lyimo (Chadema) alisema hakuna mkakati wowote
uliochukuliwa na Serikali kuhakikisha ufaulu unaongezeka, hivyo ni jambo
la kushangaza kuona matokeo yanaonyesha wanafunzi wamefanya vizuri
kiasi hicho.
“Hapo kinachooneka goli limepanuliwa ili magoli
yaingie zaidi kwani kati ya mwaka jana na mwaka huu kitu gani
kimefanyika. Ukaguzi wa walimu na wanafunzi haufanyiki, ufaulu
unaongezekaje?” alihoji Susan.
Aliongeza kuwa kinachofanyika hivi sasa ni kutaka
kuwaridhisha wazazi ambao walikata tamaa kutokana na matokeo mabaya ya
wanafunzi wao kwa miaka miwili iliyopita.
“Walimu wanajua kuwa hata wasipofundisha wanafunzi kuna mtu huko juu atawafaulisha tu,” alisema.
Mkurugenzi wa shirika la Uwezo linalojihusisha na
masuala ya elimu, Ziada Mgalla alisema wanafunzi waliofaulu wanapaswa
kupongezwa iwapo asilimia 95.98 ya ufaulu inawakilisha ufahamu wao.
Alisema historia inaonyesha kuwa wapo baadhi ya
wanafunzi ambao walifaulu kwa kiwango kikubwa lakini hawakuwa na uwezo
wa kufafanua kile walichokiandika kwenye mitihani jambo linalotia shaka
kuwa huenda matokeo ‘yalichezewa’.
“Matokeo hayo hayatakuwa na maana kama wanafunzi
waliofaulu hawawezi kuwa na ufahamu unaolingana na matokeo yao. Pia
wastani unaozungumzwa lazima mwanafunzi awe amepata kuanzia alama 60
kuendelea kama amepata chini ya hapo hakuna sababu ya kushangilia,”
alisema Ziada.
Akizungumzia sababu za shule za umma kufanya
vibaya, mkurugenzi huyo alisema kuwa Serikali ijiulize kwa nini walimu
wanaofundisha shule hizo wanafunzi wao hufeli, lakini wakienda
kufundisha shule za binafsi, wanafunzi wao hufaulu.
“Suala siyo tu kuwa na walimu, wawasikilize
wanapolalamika vinginevyo itafika wakati mwanafunzi wa sayansi
ataonekana amefaulu lakini akifika kwenye upasuaji akashindwa kufanya
kazi taifa likatia aibu,” alisema.
Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa HakiElimu,
Boniventura Godfrey alisema wakati watu wanashangilia matokeo hayo
yaliyotajwa kuwa ni mazuri yakilinganishwa na miaka iliyotangulia, wadau
wa elimu wanapaswa kujiuliza kwa nini shule za umma zilizokuwa
zikiongoza miaka ya nyuma zinazidi kufanya vibaya.
Alisema Serikali inatakiwa kuchukua hatua za haraka kukabiliana
na tatizo hilo kwa kuwa hata mazingira ya shule hizo kwa sasa
yameharibika ikilinganishwa na ilivyokuwa siku za nyuma ingawa zina
idadi kubwa ya walimu.
Godfrey alisema matokeo hayo hayana uhusiano
wowote na mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa kuwa
haiwezekani ndani ya mwaka mmoja kukawa na mafanikio ya kiwango hicho.
“Sijui matokeo haya ni mazuri kwa namna gani kwa
sababu wala BRN (Matokeo Makubwa Sasa) haiwezi kuwa na mafanikio ya
haraka namna hii.
Ninadhani suala la kuangalia hapa ni kwa nini shule za umma zimefelisha huku za binafsi zikiendelea kuongoza,” alisema.
0 Comments