FAIDA YA KUTAFUTA NA HASARA YA KUPATA

Ni watu wachache ambao wanaweza kujisifu kwa uhodari wa kutafuta. Naamini ni nadra kumkuta mtu akifurahia kubeba mzigo mzito, kulima, kufanya kazi, kujituma katika shughuli hii na ile kwa sababu kutafuta tunakuchukulia kama kero.
Ni rahisi kutamani kufanya kazi kidogo lakini si kupewa fedha au mgawo wa mafanikio kwa kiwango kidogo. Tamaa ya wanadamu wengi ni kupata na si kutafuta.
Kwa msingi huo, sioni haja ya kusubiri jibu la kipi bora kati ya kupata na kutafuta kwa sababu najua; vijana wengi wanatamani sana kupata kazi nzuri, kuwa na fedha nyingi za kufanyia anasa, mavazi ya gharama na  nyumba za kisasa. Hivyo chaguo lao ni kupata.
Kitaalamu, miongoni mwa makosa makubwa yanayofanywa na watu ni kupenda kupata na kuchukia kutafuta. Msomaji wangu, utajiri si wingi wa pesa au mafanikio bali kufanya kazi na shughuli nyingi zaidi ya mafanikio uliyopata.
Siku zote wanaofanikiwa duniani ni wale wanaopenda kutafuta, hawachoki kuwekeza, hawaachi kujitumikisha, hawatafsiri faida kama pato la kutumia kwa anasa bali nyenzo ya kuwawezesha kutafuta zaidi.
Mchanganuo wa mambo haya mawili uko hivi: KUPATA; mfumo wake ni matumizi. Mtu aliyepata mshahara akafurahi, akaridhika, hana njia nyingine zaidi ya kuutumia mshahara huo kununulia nguo, kulipia umeme, pango la chumba na ada za shule.
Ukweli ni kwamba, hata kama fedha na mafanikio aliyopata mtu yatakuwa makubwa kiasi gani kwa mfumo huu wa kutoa, matokeo tarajiwa ya siku za usoni ni kumalizika kwa pato na hivyo kumpeleka mtu kwenye hatua nyingine ya kutafuta.
Lakini KUTAFUTA; ni mrija uvutao mafanikio. Anayetafuta hupata zaidi na zaidi na uzuri wake ni kwamba, mfumo huu umeunganishwa moja kwa moja na KUPATA. Kwa msingi huo anayetafuta anakuwa sawa na mtu anayeishi ndani ya mifumo miwili kwa mpigo na kwake mtu huyo hakuna kufilisika bali apataye hufilisika.
Nashauri, watu wote tufurahi zaidi wakati wa kutafuta, tujivunie uwezo wa kutenda, tupende kazi zinazotuingizia mishahara na kamwe tusipende mishahara inayotupeleka kwenye matumizi yatakayoturudisha kwenye mfumo wa kutafuta tusioupenda.
Muhimu kuunganisha nguvu katika harakati za kutafuta maisha na kuachana na mfumo wa kushirikiana zaidi kwenye matumizi ya vile tunavyopata kwa sababu mwisho wake ni mbaya.
Nimalizie makala haya kwa kuwashukuru wasomaji wangu wote kwa kuniunga mkono katika safu hii, siku zote nafurahi kusikia jinsi ambavyo makala zangu zimekuwa zikibadilisha maisha ya watu.

0 Comments