MTU
asiyefahamika anayedhaniwa kuwa ni jambazi, amevamia basi la magereza
linalobeba mahabusu, lenye namba MT 0046 na kuwajeruhi kwa risasi askari
wawili na mahabusu mmoja maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam jana.
Waliojeruhiwa ni dereva wa basi hilo mwenye namba za kijeshi A. 9719,
askari polisi wa kike, WP 4481 Koplo Dotto na mahabusu aliyefahamika
kwa jina la Dorin Damian.
Akithibitisha tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi
Kinondoni, Kamishna Msaidizi (ACP), Camilius Wambura, alisema dereva wa
basi hilo alijeruhiwa mkono wa kulia, Koplo Dotto eneo la kifuani na
mahabusu Damian usoni.
Kamanda Wambura alisema mtu huyo ambaye hajafahamika lengo lake,
alirusha risasi katika basi hilo lililokuwa na mahabusu likitokea Kawe
kwenda mahakama nyingine, na kwamba mbali ya kusababisha majeraha, pia
amefanya uharibifu wa vioo vya basi hilo.
Wakati Kamanda Wambura akielezea hali hiyo, walioshuhudia tukio hilo
walisema watu waliokuwa kwenye pikipiki walikuwa wakilifuatilia gari
dogo ambalo lilikwama katika foleni karibu na Regency Hotel Mikocheni.
Waliongeza kuwa ghafla watu hao walianza kurusha risasi katika gari
la magereza, wakihofia mkakati wao kujulikana na askari waliokuwa
wakisindikiza mahabusu.
Tukio hilo, limekuja takribani wiki tatu, tangu majambazi wavamie
kituo kidogo cha polisi Mkuranga mkoani Pwani na kuua askari mmoja papo
hapo na kumjeruhi mgambo ambaye alifia hospitali na kuiba bunduki tano.
0 Comments