- CCM, Ukawa watupiana lawama
Mdahalo huo uliitishwa kujibu swali hilo ambalo
limekuwa likiulizwa na Watanzania wengi, hasa baada ya wabunge wa vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia mjadala wa
Bunge la Katiba, wakidai CCM inataka kujadili rasimu yao badala ya ile
iliyowasilishwa kwenye bunge hilo na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ukawa wamekuwa wakisisitiza kuwa hawatarejea
kwenye Bunge la Katiba linalotarajia kuanza Agosti 5, mwaka huu hadi
watakapothibitishiwa kwamba majadiliano yatakuwa yakiihusu Rasimu ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph
Warioba.
Mdahalo huo ulikuwa ukiongozwa na Mwanyekiti
Mtendaji wa EABMI, Rose Mwakitwange na uliwakutanisha wazungumzaji wakuu
ambao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen
Wassira, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Profesa Ibrahim
Lipumba.
Wazungumzaji hao walitoana jasho wakati wakijibu
swali hilo na mustakabali wa Mchakato wa Katiba, hasa kuhusu muundo wa
muungano.
Profesa Lipumba anaanza kujibu swali hilo kwa
kueleza kuwa wahafidhina wa CCM, ndiyo waliokwamisha upatikanaji wa
Katiba Mpya. Anasema Rais Kikwete alikuwa na nia njema ya kuwapatia
Watanzania Katiba Mpya, lakini wahafidhina wa CCM hawataki wananchi
wapate katiba yenye maoni yao.
“Kikwete alikuwa na nia njema ya kuwapatia
Watanzania Katiba Mpya, lakini wapo wanachama wa CCM ambao hawataki
mabadiliko ili kulinda masilahi yao,” anasema.
Lipumba anadai kuwa Wahafidhina wa CCM
wamefanikiwa kumshawishi rais na akaanza kuiponda Rasimu ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na kusababisha mchakato huo kuingia dosari.
“Kwa hiyo ili kujibu swali hilo ni kwamba CCM ndiyo wanaokwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya,” anasema.
Kwa upande wake Waziri Wassira anasema
wanaokwamisha upatikanaji wa Katiba mpya ni wale wanaojiita Ukawa
waliosusia vikao vya bunge kwa kutoka nje ya ukumbi.
“Katiba Mpya haiwezi kujadiliwa katika eneo la
Kibandamaiti au katika viwanja vya Jangwani. Katiba inaandikwa bungeni,
wenzetu Ukawa wamekimbia,”anasema.
Wassira anasema, “Njooni bungeni tuandike Katiba
ili tuwaachie wananchi waamue katika kura ya maoni, wao ndiyo wenye
uamuzi wa mwisho.
Wassira anasema Bunge la Katiba lina uwezo kisheria kubadilisha
mambo yaliyomo kwenye Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba tofauti na
madai ya Ukawa kuwa halina uwezo huo.
“Ni lazima nieleze wazi kwamba Bunge la Katiba
haliwezi kupitisha kila jambo lililowekwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, kuna mambo tutayabadilisha na hiyo ndiyo kazi ya Bunge,” anasema
Wassira.
Anasema haiwezekani bunge lenye wajumbe 629 liwe
na kazi ya kupitisha kila kilichomo kwenye rasimu, vinginevyo uwepo wake
hauna maana.
“Kama ni hivyo basi bunge hilo lingeweza kukaa kwa wiki moja na kumaliza kazi hiyo kwa sababu ni kazi rahisi sana,” anasema.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anasema
wanaoyapinga maoni ya wananchi yaliyopo kwenye rasimu, ndiyo hawana nia
njema na Katiba mpya.
“Katiba ni ya wananchi, huwezi kupuuza maoni yao
halafu useme una nia njema ya kutaka Katiba mpya, CCM wanataka Katiba
yenye maslahi kwa vigogo wachach,” anasema.
Lissu anasema ili kufanikisha lengo lao, kati ya
wajumbe 201 walioteuliwa kuwakilisha makundi mbalimbali, wajumbe 166 ni
wanachama wa CCM ambao waliteuliwa kwa lengo la kuongeza nguvu.
“Ndiyo maana sisi tumeamua kutoka bungeni ili
tusishiriki katika uovu huo, tunafahamu kabisa CCM lengo lao ni kuandaa
katiba ile ile lakini yenye rangi tofauti,” anasema.
Wajumbe wa tume
Wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Humphrey Polepole na Awadhi Nassor Said, wakasema Wajumbe wa
Bunge la Katiba ambao ni wanachama wa CCM, waliukejeli mchakato huo,
hivyo hawana nia njema na mustakabali wa taifa.
Awadhi anasema Tume ya Jaji Warioba ilikusanya
maoni ya wananchi katika wilaya 143, ikifanya mikutano 12 katika kila
wilaya ya Tanzania bara na 22 Zanzibar, hivyo ikafanya jumla yake kuwa
1,700.
Anasema kulikuwa na mabaraza ya katiba 177 na
kwamba asasi za kiraia 614 ziliunda mabaraza ambayo wajumbe wake hivyo
wajumbe wake wakafanikisha kupatikana kwa rasimu, iweje misingi yake
ipinduliwe na watu 629.
“Tume ilichukuwa sampuli ya maoni sasa kama wao CCM wanasema
wanaotaka serikali tatu ni wachache wao wanataka serikali mbili kwa
takwimu zipi,” anasema.
Polepole anaionya CCM juu ya mpango wa
uchakachuaji wa rasimu hiyo halisi, huku akiwaasa Watanzania kufuatilia
mchakato huo kwa makini.
Mchakato uahirishwe hadi 2016
Wakati huohuo Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata),
limependekeza Bunge la Katiba kuahirishwa hadi mwaka 2016, baada ya
uchaguzi mkuu.
0 Comments