ufupi
Pia, endapo mwenye nyumba ndani ya miezi sita
atakuwa hajafanyia marekebisho basi mpangaji ana haki ya kuvunja mkataba
na kudai fidia lakini anapaswa kutoa notisi ya mwezi mmoja kabla ya
kufanya hivyo.
Ardhi ni kitu muhimu sana katika maisha ya kila
siku ya binadamu. Hata hivyo, ukweli ni kwamba siyo kila Mtanzania
anamiliki ardhi.
Wengi wamepanga kwenye nyumba au maeneo ya watu wengine.
Wiki iliyopita tuliangalia kwa kina majukumu ya
mpangaji, leo tutajikita zaidi kwenye haki za mpangaji na majukumu ya
mwenye nyumba.
Sheria inayosimamia haya ni pamoja na ile ya ardhi
ya mwaka 1999, sheria ya usajili wa ardhi sura ya 334, kesi mbalimbali,
mkataba wa pango pamoja na sheria zingine zote za nchi.
Sheria imeweka haki hizi na majukumu kwa mwenye nyumba na inapaswa ziheshimike. Sheria na majukumu haya zinapaswa kuzingatiwa.
Endapo mpangaji kalipa kodi yake vizuri na
anaheshimu mkataba waliojiwekea, ana haki ya kutumia eneo/nyumba hiyo
kwa kipindi chote cha muda wa mkataba bila bughudha ya aina yoyote
(peaceably and quietly possess and enjoy the land leased). Hii ni kwa
mujibu wa kifungu cha 88 (1) (a) cha Sheria ya Ardhi Sura ya 113.
Kupewa taarifa kuhusu upekuzi wowote
Endapo mwenye nyumba anataka kufanya upekuzi wa
aina yoyote kwenye nyumba ya mpangaji, anatakiwa na sheria kutoa taarifa
hii mapema.
Haki ya kupata nyumba ambayo ipo katika hali nzuri
anayoweza kuishi binadamu (fit for human habitation) kwa kipindi chote
cha mkataba, kwa hiyo mwenye nyumba ana jukumu hilo kisheria, siyo leo
mtu amepanga kesho ukuta umebomoka hiyo nyumba haitakuwa katika hali
nzuri. Ni jukumu la mwenye nyumba kuirekebisha. Hii ni kwa mujibu wa
kifungu cha 88 (1) (d) cha Sheria ya ardhi Sura ya 113.
Mwenye nyumba kutotumia ardhi ya jirani au sehemu
yoyote ya ardhi itakayo athiri matumizi ya ardhi iliyokodiwa; kwa mfano
mtu anapanga leo eneo kama sehemu ya kufundishia, baada ya wiki unakuja
kufunga mashine jirani na hapo inayopiga kelele muda wote kiasi cha eneo
lilipongwa linakuwa halina maana tena.
Mwenye nyumba kufanya matengenezo pale nyumba
inapoharibika au kubomoka na kufanya kuwa siyo sehemu ya kuishi binadamu
wa kawaida, ikibomoka kwa radi, mvua, mafuriko,upepo mkali n.k. Hii ni
kwa mujibu wa kifungu cha 88 (1) (e) cha Sheria ya Ardhi Sura ya 113.
Pia, endapo mwenye nyumba ndani ya miezi sita
atakuwa hajafanyia marekebisho basi mpangaji ana haki ya kuvunja mkataba
na kudai fidia lakini anapaswa kutoa notisi ya mwezi mmoja kabla ya
kufanya hivyo.
Mwenye nyumba pia ana jukumu la kulipa kodi ya jengo na kodi
zingine zinazohusiana na nyumba hiyo.Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 88
(1) (g) cha Sheria ya ardhi Sura ya 113. Mfano kodi ya jengo n.k. Bili
za umeme na maji na makubaliano baina ya pande mbili mpangaji na mwenye
nyumba.
Pia, mpangaji anaweza kuvunja mkataba endapo
ataona eneo/ nyumba aliyopanga haifai tena kwa matumizi kama yale ya
awali, kwa mfano mtu amepanga kwa ajili ya kuendesha mashine yake lakini
baadaye umeme wanakata kwa kosa la mwenye nyumba, kisheria huyu
mpangaji hawezi kuendelea na hilo eneo, anaweza kutoa notisi ya mwezi
mmoja na kuvunja mkataba.
Kimsingi hizi haki lazima ziwepo kwa kila mkataba, na mikataba lazima iwe imeandikwa kisheria na inayokubalika.
Mwandishi wa makala hii ni Jebra Kambole Wakili wa Kujitegemea kutoka Kampuni ya Law Guards Advocates wa jijini Dar es Salaam.
0 Comments