Dk. Slaa pia aliwataka Watanzania wote hususani jamii za wakulima na wafugaji kuacha kupigana na kuuana wakigombea ardhi badala yake waiwajibishe Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuwa migogoro hiyo ni matokeo ya serikali hiyo kushindwa kuwajibika ipasavyo hasa katika kuweka mipango mizuri ya matumizi ya ardhi ambayo ni majukumu ya Serikali za Mitaa.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara ya chama hicho iliyopewa jina la ‘Operesheni Delete CCM’ akimpokea Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, aliyezunguka mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma na Morogoro.
Alisema kuwa migogoro ya ardhi inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha umwagaji damu za Watanzania na uharibifu mkubwa wa mali ni matokeo ya kushindwa kwa sera, mipango na mikakati ya CCM, hivyo akawataka wananchi kujiandaa kukipumzisha chama hicho kutoka madarakani.
Akizungumza katika mkutano wake wa kwanza kijijini Mvuha, kati ya mikutano mitano kwenye vijiji mbalimbali vya majimbo ya Morogoro Kusini, Morogoro Kaskazini na Kilosa, Dk. Slaa alisema kuwa umwagikaji wa damu huo usipodhibitiwa na migogoro hiyo kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu, serikali itakuwa imeshindwa moja ya majukumu yake ya msingi ya kulinda raia wake.
“Ndugu zangu, ziara hii itanifikisha katika maeneo ambayo mnajua yamekuwa na migogoro ya ardhi…kumekuwepo na migogoro hata huku kwenu isiyokwisha ya wakulima na wafugaji kugombea ardhi…Mkoa wa Morogoro baraka ya ardhi na utajiri wa rutuba mliopewa umekuwa ukigeuka laana kiasi cha damu za watu kumwagika.
“Yanatokea sana huko Mvomero, Kilosa hata hapa kwenu (Mvuha) nimeambiwa migogoro ipo. Tunavyozungumza hivi sasa kuna matukio ya kutisha yametokea huko Kiteto, Siha, Malinyi na kwingine. Ndugu zangu, wakulima na wafugaji…ninyi wote ni Watanzania. Nawaomba sana muendelee kuishi kama ndugu kama ilivyokuwa huko nyuma,” alisema.
Dk. Slaa aliongeza kuwa hayo ni matokeo ya serikali kushindwa majukumu yake na vile vile kushindwa kwa sera za CCM, mipango na matumizi mazuri ya ardhi.
Alisema kuwa ili ardhi ya mifugo na kilimo ijulikane na matumizi mengine ni kazi za Serikali za Mitaa kupitia halmashauri, hivyo akawasihi wananchi kuwa huko kote sera za CCM zimeshindwa, kwamba ndio maana wanasema ‘delete CCM’.
“Kupitia mkutano wangu huu leo tunaitaka serikali ya Kikwete ichukue hatua za haraka sana kuzuia umwagaji wa damu unaoendelea na kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa migogoro ya ardhi nchini. Vinginevyo wanazidi kudhihirisha kuwa wamechoka na watakiwa kupumzishwa.
“Kwa Kiteto mojawapo ya chanzo cha mauaji yanayoendelea huko ni wanasiasa wanaoongoza wilayani humo, akiwemo Mkuu wa Wilaya, yuko Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, yupo mbunge wa jimbo ambaye amewahi kuwa waziri…mgawanyo wa ardhi ni jukumu la serikali. Hatuwezi kuangalia tu damu ya Watanzania inamwagika kama kuku. Hatuwezi. Tunamtaka Kikwete amfukuze kazi huyo DC,” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa iwapo viongozi walioko madarakani sasa hawataona thamani za damu zinazomwagika kwa sababu ya wao kushindwa kutekeleza wajibu wao, iko siku watailipa kwa gharama kubwa endapo wananchi wataendelea kupoteza matumaini huku haki ikiwa haipatikani, huku akisisitiza kuwa hayo yataanza kuonekana kuanzia uchaguzi wa Desemba 14 mwaka huu.
Dk. Slaa ambaye jana alifanya mikutano katika vijiji vya Mvuha, Kisika, Ludewa, Magubike na akimaliza mkoa wa Morogoro akiingia mkoani Dodoma leo, aliwataka Watanzania katika jamii zao, zikiwemo za wakulima na wafugaji, kuacha kuuana wao kwa wao, badala yake wajue namna ya kushughulikia chanzo cha migogoro yao.
0 Comments