Kwa ufupi
- Kauli hizo zimejitokeza baada ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), kutangaza ufaulu wa wanafunzi 451,392 kati ya 808,085 waliosajiliwa kufanya mtihani.
Dar es Salaam. Wadau wa elimu
nchini wamekosoa ufaulu wa matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa juzi
kwa kusema siyo ishara ya kukua kwa sekta hiyo, ilhali kuna tatizo la
kisera.
Kauli hizo zimejitokeza baada ya Baraza la
Mitihani Tanzania (Necta), kutangaza ufaulu wa wanafunzi 451,392 kati ya
808,085 waliosajiliwa kufanya mtihani.
Katika ufaulu huo, somo la Kiswahili linaongoza
kwa asilimia 69.70, huku Kiingereza kikiwa ni asilimia 38.84,
ikilinganishwa na asilimia 35.52 za mwaka jana.
Katibu mtendaji wa Jumuiya ya Wamiliki wa Shule na
Vyuo Binafsi nchini (TAMONGSCO), Benjamin Nkonya alisema matokeo hayo
ni maandalizi ya wanafunzi kuanguka kimasomo katika ngazi ya sekondari
kwa kuwa watafundishwa kwa Kiingereza, lugha ambayo wengi hawaijui.
“Somo walilofeli ni Kiingereza, ambalo ndiyo
msingi wa kufaulu kwa ngazi ya sekondari. Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa
(BRN) unaweza kuwa mbwembwe tu, kwani tatizo hilo limekuwa la kisera,”
alisema na kuongeza:
“Hata mipango ya awali ya Upe (Elimu ya Msingi kwa
Wote) na MMEM (Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi) haikuonyesha
mafanikio yoyote, matokeo yake wanafunzi wanaotoka daraja hilo wanaishia
kupata alama ‘0’ kwa kudhani ni wajinga kumbe hawakuwa na uelewa wa
lugha ya kufundishia.”
Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe
alisema pamoja na udhaifu wa matumizi ya lugha, kiwango hicho cha ufaulu
siyo ishara ya mafanikio.
Profesa Shumbusho alihoji inakuwaje wanaofaulu baadhi yao huwa hawafikii vigezo vya kuingia ngazi ya elimu ya sekondari.
“Wamefaulu nusu, lakini utakuta wengi wanaingia
kidato cha kwanza hawajui kusoma na kuandika, hawana uwezo na ufahamu wa
kutosha katika masomo? bado inatia shaka sana na wingi huo wa ufaulu,”
alisema.
“Mbali na hilo, hata wale wanaoshindwa kuendelea
na kidato cha kwanza wamejengewa uwezo gani katika masomo ya stadi za
kazi ili kujitegemea kwa kazi za kujiajiri?”
Mhadhiri mwandamizi wa Idara ya Saikolojia na
Mtalaa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Eugenia Kafanambo alisema
siyo sahihi kuhukumu matokeo hayo kwa sasa, kabla ya kuona uwezo wa
wanafunzi hapo baadaye.
Eugenia alisema mpango wa BRN unaweza kuwa sababu ya ufaulu huo kutokana na walimu kujizatiti katika utekelezaji wake.
“Kama watakuwa wamefaulu kwa ujanjaujanja, lazima itafahamika tu
wakati watakapoanza majaribio katika masomo yao ya awali... Taarifa
tutazipata tu,” alisema na kuongeza kuwa uchakachuaji wa mitihani kwa
ngazi ya Necta umepungua ila hofu inaweza kuwa katika halmashauri.
Profesa Kaahyarara Godius kutoka UDSM, alisema
ushindani katika halmashauri na shule vinaweza kuwa sehemu ya mchango
mkubwa uliosababisha ufaulu huo.
0 Comments