WATANZANIA TUACHE KUSHABIKIA MAMBO YASIYO NA FAIDA

 
 
Kwa ufupi
Watanzania acheni kushabikia mambo yasiyo na faida


Nianze kwa kuwapa salamu Watanzania wenzangu mliojaa uzalendo, mlio tayari kuhoji mambo ya msingi kwa mustakabali wa nchi yetu.
Nawapongeza kwa sababu mnajitambua na angalau mnaweza kuwatia kashikashi viongozi wa Serikali pale ambapo wanasahau majukumu yao.
Nia yangu si kuponda tabia za baadhi ya Watanzania wenzagu ‘waliolala’, lengo langu ni kuwapa ushauri tu kwamba hata kama wanashabikia mambo yasiyo na faida katika maisha yao, wakumbuke kuwa kuna mambo ya muhimu yanahitaji kupigiwa kelele kama si kupingwa.
Wananchi ndio wenye nchi, hivyo wanapaswa kuhakikisha kuwa nchi yao ipo katika njia sahihi. Hata nchi zilizoendelea zilifikia hatua hiyo baada ya wananchi wake kujitambua.
Hapa kwetu Tanzania baadhi ya wananchi wamekuwa mahodari kuhoji na hata kufuatilia, mambo ambayo hayawezi kuwasaidia hata kupata mlo wa usiku tu.
Kila mtu analikumbuka lile sakata la Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu. Mwanadada huyu aliyetwaa taji la urembo, anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kudanganya umri wake, kitu ambacho ni kinyume na kanuni za mashindano hayo ya urembo.
Sakata hilo lilikuwa mjadala katika mitandao ya kijamii, vijiweni, katika daladala na hata kwenye baadhi ya maofisi.
Ni kweli kabisa mrembo huyo wa Tanzania anakwenda kuiwakilisha nchi, lakini tujiulize nguvu iliyotumika kumpinga Sitti ina faida gani kwa wananchi maskini.
Umejaribu kufikiri Miss Tanzania inasaidiaje kuboresha maisha yako na wananchi wengine walioko vijijini. Miss Tanzania inaweza kuleta huduma bora za afya?
Vipi kuhusu elimu, unadhani Miss Tanzania inaweza kuisaidia nchi kujenga mabweni, maabara, kununua madawati. Jibu ni hapana.
Mambo niliyoyataja hapo juu ni baadhi tu yanayotakiwa kupigiwa kelele na idadi kubwa ya Watanzania ili kuifanya nchi yetu iweze kupiga hatua kama nchi nyingine ambazo miaka 1960 zilikuwa hazina tofauti ya kiuchumi na Tanzania.
Sikatai watu kumpinga, kinachonishangaza ni tabia ya walio wengi ya ‘kushupalia’ jambo hili au mengine yanayofanana na hilo huku wakiacha kujadili mengine ya msingi.
Wakati mwingine tunailaumu Serikali yetu kuwa haijafanya hili au lile na kusahau kuwa tuna swali la msingi tunatakiwa kujiuliza kuwa tumeifanyia nini Tanzania?
Kuipigania nchi yako ni pamoja na kuhoji juu ya ufisadi wa mabilioni ya fedha, kuhoji zilipo fedha za ujenzi wa maabara, shule, mabweni na hata hospitali.
Tuhoji juu ya ahadi za wagombea, ubovu wa barabara, wizi na rushwa inayotafuna nchi yetu. Tuwanyooshee vidole viongozi wanaoshindwa kuwajibika tena kwa nguvu ile ile tunayoionyesha katika facebook, twitter, instagram na WhatsApp.
Wapo baadhi ya watu wanakesha vijiweni kudadisi maisha ya wenzao huku wengine wakitaka kuishi kama ‘wenyenazo walioko majuu’ wakati ni vinara kukesha baa.
Hatuwezi kubadili nchi yetu na maisha yetu kama tutaikumbatia tabia ya kushabikia yasiyo na faida.

0 Comments