Hivi kwa nini walimpa dhamana wakati alishatoroka mara ya kwanza, na
huyu mwandishi aliyemdhamini najua hamfahamu lakini amejiingiza kwenye
matatizo ya kujitakia. James Lembeli
Kwa ufupi
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mfawidhi wa mahakama
hiyo, Simon Kobelo, ambaye pia aliamuru kutaifishwa kwa mali zote za
mtuhumiwa huyo zilizopo katika ardhi ya Tanzania.
Moshi/Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mkoa wa Kilimanjaro, jana imemhukumu raia wa Pakistan Ahmed
Kamran kifungo cha miaka 60 jela baada ya kumtia hatiani kwa makosa
manne ikiwamo kusafirisha twiga wanne hai kwenda Qatar.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mfawidhi wa
mahakama hiyo, Simon Kobelo, ambaye pia aliamuru kutaifishwa kwa mali
zote za mtuhumiwa huyo zilizopo katika ardhi ya Tanzania.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana baada ya
kutolewa hukumu hiyo, Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji
Peter Msigwa alisema kilichofanyika ni kutaka kuonyesha haki imetendeka,
huku Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira,
James Lembeli akisema kuwa kumsaka mtuhumiwa huyo ni sawa na mchezo wa
kuigiza.
Hata hivyo, tayari Shirika la Polisi la Kimataifa
(Interpol) juzi limewataka Watanzania kusaidia katika kumsaka Kamrani,
huku likitangaza kuanzisha operesheni iliyoipa jina la Infra Terra
ikilenga kuwanasa watuhumiwa uharamia zaidi ya 139 katika nchi 36
duniani.
Mchungaji Msigwa alisema kuwa kilichofanyika ni
kiini macho kwa kutaka kuonyesha kuwa haki imetendeka. Alisema
haiwezekani Ahmed apatikane na kosa pekee yake wakati mchakato wa
kusafirisha wanyama unaonyesha watu wengi wakiwamo viongozi walishiriki
kutekeleza biashara hiyo.
“Hata kama wangemfunga miaka 200 haisaidii kitu,
hapo mahakama imefanya kazi yake lakini Serikali inafanya kiini macho,”
alisema Msigwa.
Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini,
alisema kitendo cha mahakama kuthibitisha kuwa mfanyabiashara huyo
alikuwa na vibali halali kinaonyesha kuwa kuna baadhi ya watu
walishiriki kumtorosha ili wasitiwe nguvuni.
“Isingewezekana ndege iingie nchini bila wakubwa kujua ilikuja kufanya nini?” alihoji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili
na Mazingira, James Lembeli alisema kumsaka mtuhumiwa Kamran Ahmed
anaona huo ni mchezo kwa sababu mtuhumiwa huyo raia wa Pakistan
alishatoroka awali kisha akapatikana, lakini katika hali ya kushangaza
akapewa tena dhamana.
Lembeli alisema hatua ya kuruhusu dhamana ya pili
kwa mtuhumiwa huyo inatia shaka kuwa kuna jambo lisilo la kawaida
lililomwezesha kutoroka kwake.
“Hivi kwa nini walimpa dhamana wakati alishatoroka
mara ya kwanza na huyu mwandishi Temba aliyemdhamini sijui alianzia
wapi, najua hamfahamu lakini amejiingiza kwenye matatizo ya kujitakia,”
alisema Lembeli.
Kuhusu ndege inayodaiwa kutumika kusafirisha
wanyama hao, ambapo mahakama imethibitisha kuwa ilikuwa na vibali vyote
halali vya kuingia nchini kwa safari ya kidiplomasia, Lembeli alisema
Wizara ya Mambo ya Nje ieleze kwa kina jambo hilo lilitokeaje.
“Mimi katika hilo sitaki kuzungumza sana, ila nafikiri kuna haja
ya kujiridhisha kuwa kibali hicho cha kidiplomasia ni cha aina gani,
kilitolewaje, kisha majibu tutakayopata ndipo tutajua nini kilitokea,”
alisema Lembeli.
Alipotafutwa kwa njia ya simu, Waziri wa Maliasili
na Utalii, Lazaro Nyalandu na naibu wake, Mahmoud Mgimwa, simu zao
ziliita bila kupokelewa.
Hukumu ya kesi hiyo ilitolewa bila mtuhumiwa wa
kwanza (Kamran) kuwapo mahakamani baada ya kutoroka tangu Februari mwaka
huu wakati kesi yake ikiwa katika hatua za mwanzo za usikilizwaji.
Katika hukumu hiyo, hakimu Kobelo aliwaona
washtakiwa wengine wanne, Hawa Mang’unyuka, Martin Kimath na Michael
Mrutu kuwa hawana kesi ya kujibu na kuwaachia huru.
Hakimu Kobelo alisema hakuna ubishi kuwa raia huyo
wa Pakistan (Kamran), ndiye aliyekuwa wakala katika biashara hiyo na
ambaye ndiye aliyewasafirisha wanyama hao kwa kutumia ndege kubwa ya
Jeshi la Qatar. Kobelo alisema ndege hiyo ilikuwa na vibali vyote halali
vya kuingia nchini kwa safari ya kidiplomasia kupitia Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Kilimanjaro(KIA).
Hakimu Kobelo alisisitiza kuwa ndege iliyobeba
wanyama hao ilikuwa na hadhi ya kidiplomasia na ilifuata taratibu zote
na kuruhusiwa na mamlaka za nchi ikiwamo Wizara ya Mambo ya
Nje.Uchambuzi wa ushahidi huo unaonyesha raia huyo wa Pakistan,
aliruhusiwa na mamlaka za Tanzania kukamata wanyama kwa kutumia leseni
za kampuni mbili zinazomilikiwa na Hawa.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo hakuwa na kibali cha
kusafirisha wanyama hao kwenda nje ya nchi na kwa kuwa alitoroka,
mahakama haikuweza kupata uthibitisho wake kama alikuwa na kibali.
Kutokana na uchambuzi huo, mahakama imemtia
hatiani raia huyo wa Pakistani kwa makosa manne ambapo kila kosa
amehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.
0 Comments